kitaifa

Bulaya hashikiki, amlipua Wassira

Friday, July 24 2015, 0 : 0


ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi.Esta Bulaya ambaye juzi alitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amepata mapokezi makubwa Mjini Bunda jana akitokea jijini Mwanza akiwa na viongozi wa CHADEMA mkoani humo na Kanda ya Ziwa.

Akiwahutubia wananchi katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Bi.Bulaya aliwapongeza wananchi kwa mapokezi makubwa waliyompa na kumlipua mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Bw. Stephen Wassira akisema muda wake wa kukaa serikalini unatosha.

Alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano, viongozi kama Bw. Wassira hawafai kwani amekuwa Waziri muda mrefu lakini jimbo hilo bado halina maendeleo yaliyotarajiwa na wananchi.

"Wazazi wangu mimi ni mwanachama wa CCM na mimi nimekulia ndani ya chama hicho hivyo mkiona nimekimbia, mjue mambo yamenifika shingoni, katika mkoa huu kuna rasilimali nyingi ambazo hazijatumika vizuri ili ziwaondolee wananchi umaskini," alisema.

Akizungumzia uwazi na uwajibikaji, alisema viongozi wengi wa CCM hawataki kuwatetea wananchi na kushindwa kuwasimamia watendaji wa Serikali akitolea mfano mradi mkubwa wa maji mjini humo ambao umechukua miaka tisa bila Bw.Wassira kuukamilisha.

"Leo hii Wassira atakuja na sera gani kwa wananchi wakati ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mbunge na kiongozi wa Serikali, tuwakatae viongozi wa ngazi zote wanaotokana na CCM," alisema.

Aliongeza kuwa, umefika wakati wa majimbo yote mkoani humo kuchukuliwa na wagombea wa CHADEMA ambao watatimiza ahadi zao kwa wananchi na kutatua kero walizonazo.

Bi.Bulaya aliweka wazi dhamira yake ya kuwania ubunge wa Bunda Mjini kwa tiketi ya CHADEMA ambapo leo atashiriki kura ya maoni ya kumpata mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA.

Naye mbunge wa Kahama, Bw. James Lembeli, alidai kuchoshwa na ufisadi uliopo ndani ya CCM na kuwataka wananchi wakubali kuiunga mkono CHADEMA kwa kuwaweka madarakani na kushika dola katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Mbunge wa Musoma Mjini, Bw. Vicent Nyerere, alilitaka Jeshi la Polisi kutoa ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu na kuacha kuitetea CCM huku akidai jeshi hilo ni sehemu ya Watanzania ambao wote wamepigika.

chadema yafunika mwanza

Thursday, July 23 2015, 0 : 0


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetikisa Mkoa wa Mwanza kupitia mkutano wake wa hadhara uliohudhuriwa na umati mkubwa wa watu, huku kikiwataka Watanzania kuendelea kuwa wavumilivu kuhusiana na suala la kumjua mgombea wa UKAWA.

Mkutano huo uliofanyika jana kwenye viwanja vya Magomeni Ilemela, uliohutubiwa na viongozi wa kitaifa pamoja na wabunge. Mbali na viongozi hao, pia mkutano huo ulitumika kuwatambulisha makada wapya waliohamia chama hicho kutoka CCM.

Waliotambulishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ni aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Esther Bulaya na James Lembeli, ambaye alikuwa mbunge wa Kahama.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe mbali ya kuwakabidhi kadi na kuwaombea msamaha kwa waliyoyafanya wakiwa CCM,  aliwataka wananchi kuwa wavumilivu katika suala zima la kumpata mgombea kupitia UKAWA kwa kuwa majadiliano yanaendelea vizuri.

"Tunaomba tuwe watulivu kwani umoja wetu unaendelea vizuri, lakini hatutampata mgombea kwa sababu eti CCM wamemtangaza mgombea wao, bali tutampata mgombea wetu kwa kukubaliana," alisisitiza Mbowe.

Alisema wako imara na wataendelea kushikamana licha ya changamoto zinazoukumba umoja huo, kwani wao kama viongozi watahakikisha UKAWA inasimamisha mgombea mmoja kwenye Uchaguzi Mkuu.

Alisema kwa sasa wanaendelea kumalizia mambo madogo madogo yaliyobaki ili kuweza kufikia mwafaka hivyo wananchi waendelee kuwaamini.

Alisema sio kwamba baadhi ya viongozi wa wanaounda umoja huo wameshindwa kutokea katika Mkutano huo bali aliwasiliana nao lakini kutokana na kuwepo kwa vikao katika vyama vyao ndio maana wameshindwa kufika.

Alisema hatakubali kuona haki haitendeki katika Uchaguzi Mkuu ujao hata kama wenzao watatumia mabavu.

Alisema ikiwa haki itatendeka katika Uchaguzi Mkuu ujao wao hawatakuwa na tatizo lakini kukiwa na ukiukwaji wa taratibu basi hawatakubali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara, John Mnyika alisema UKAWA wanasubiri Baraza Kuu la Taifa la Uongozi (CUF) wakae Julai 25,2015 na baada ya hapo ndipo watatangaza Rais ambaye anakubalika na Watanzania wote.


Naye Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu,amewataka wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wasikubali kwa kabila mgombea Urais wa CCM, Dkt.John Magufuli,kwa sababu kabila ni CCM.
 
Alisema Magufuli aliuza nyumba za Serikali,alifanya biashara nchi nzima, yeye na kabila lake CCM ndiyo wanaoitesa nchi, hivyo Oktoba 25 ikifika wananchi wa Mwanza 'wamshughulikie'.
 
“Nimefanya mikutano Kanda ya Ziwa kwa wiki moja sasa nikaambiwa makabila ya Magufuli kuwa ni Mzinza, baba Msubi,mama Msukuma. Wengine wanasema Baba yake Mzinza, Mama Msubi, mara baba Mzinza. Ninamfahamu Magufuli kabila yake ni M-CCM, kabila ile ile la mafisadi wa  EPA, Escrow," alisema.
 
Alisema wakati wa wizi wa EPA, Escrow na operesheni tokomeza, waliua watu wasio na hatia, lakini Magufuli alikuwa upande wa CCM.
 
Ezekia Wenje, alisema tatizo la nchi yetu ni mfumo mbovu uliowekwa na CCM na kuwataka wananchi kutoachagua mtu kwa ukabila bali wa kuwavusha.

Kwa upande wake Katibu Mkuu CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, alisema chama hicho kiko makini na hakitameguka kama ambavyo watu wanaeleza kwenye mitandao ya kijamii  bado wanaendelea  na kazi ya  utekelezaji wa  kadi.

"Tunataka Watanzania wawe na imani na chama chetu, kwani sasa tumejipanga vizuri kuchukua  dola Oktoba 25, mwaka huu," alisema.

Alisema  watahakikisha  wanasimamia taifa  ili liweze kurudi mikononi  mwa wananchi, kwani sasa CCM imepora madaraka ya wananchi.
 
Naye Jemsi Lembeli baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema  na Mwenyekiti wa  chama hicho  alisema kuwa  alikotoka ameaga hajaenda hivihivi na hachomoki mtu safari hii.

 • Kashfa ya rushwa CHADEMA

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  MCHAKATO wa kumpata mgombea ubunge, Jimbo la Bariadi, mkoani Simiyu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), juzi uliingia dosari baada ya mkutano wa kumpata mgombea kuvunjika.

  Mkutano huo ulivunjika baada ya viongozi wa chama hicho Wilaya na wasimamizi wa uchaguzi huo, kubaini vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wagombea dhidi ya wajumbe ili waweze kuwapigia kura.

  Baadhi ya wapambe wa wagombea walikuwa wakigawa fedha waziwazi kwa wajumbe wa mkutano huo ambapo baadhi ya wapambe hao walikamatwa na vijana wa ulinzi wa CHADEMA (Red briged).

  Vijana hao walionekana wakiwashikilia wanawake wawili (majina tunayahifadhi) na mpambe wa mgombea mmoja (jina tunalo) ambao walipelekwa kwenye chumba maalumu ukumbini hapo kuhojiwa.

  Vitendo hivyo vilisababisha mkutano huo kuvunjika ambapo waandishi wa habari walizuiliwa kusikiliza mahojiano kati ya Red briged na baadhi ya wapambe wa wagombea ambao walikamatwa wakigawa fedha sh.20,000 kwa kila mjumbe aliyekuwepo ukumbini.

  Baada ya kuhojiwa, Mpambe wa mgombea ubunge alipozungumza na waandishi, alisema alikuwa akitoa fedha kwa watu waliomuomba awanunulie maji ya kunywa si kuwapa rushwa kama inavyodaiwa.

  "Kuwanunulia maji watu waliomuomba si rushwa bali ni upendo, mimi si mgombea bali nilikuwa naonesha upendo kwao, naomba waandishi msiiandike habari hii kwani itanichafua mimi binafsi na mgombea wangu," alisema mpambe wa mgombea huyo.

  Msimamizi wa uchaguzi huo, Bw. Emmanuel Mbise alithibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo kwa wagombea na kusema kitendo hicho kinachafua taswira nzuri ya chama ambacho kinapiga vita rushwa.

  Alisema baada ya kugundua uwepo wa vitendo vya rushwa, kutokana na mamlaka aliyonayo pamoja na kusikiliza ushauri wa viongozi wa chama Wilaya, waliamua kuuvunja mkutano huo ili waweze kufanya uchunguzi na kuwabaini waliohusika.

  "Watu watano walikamatwa na kuhojiwa baada ya kukutwa wakigawa fedha kwa wajumbe na baada ya kuhojiwa, walisema zilikuwa za baadhi ya wagombea ambao ndio waliowatuma.

  "Tumewakuta na fedha nyingi wakizigawa kwa wajumbe kuanzia sh.15,000 hadi sh. 20,000...mkutano huu ulikuwa na wajumbe 700 hivyo tumeuvunja ili tufanye uchunguzi kwanza, wote ambao watabainika watachukuliwa hatua kali, uchaguzi utatangazwa baadaye," alisema.

  Aliongeza kuwa, hakutegemea wagombea kugawa fedha kama karanga kwa wajumbe hao, wengine wakinunuliwa chakula na chai ambapo baada ya uchaguzi kuahirishwa, baadhi ya wajumbe walipinga uamuzi huo na kudai ni matumizi mabaya ya fedha za chama wakitaka aliyekutwa na fedha akamatwe lakini mkutano uendelee.

  "Mkutano ulipaswa kuendelea ili kumpata mgombea kwani baadhi yetu tunatoka mbali...pia mkutano huu umetumia fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi," alisema Simea Makungu lakini baadhi ya wajumbe hao walifurahishwa na uamuzi wa kuvunja mkutano huo na kuonesha chama kinataka haki itendeke kwa wagombea wote.

  Mbali ya kuvunjika mkutano huo, hakuna kiongozi wa Wilaya au Mkoa kutoka CHADEMA aliyetangaza lini mkutano huo utafanyika lakini vikao mbalimbali vilikuwa vikiendelea kujadili hali hiyo ambayo ilisababisha mkutano kuvunjika.

  Wagombea 12 ndio waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ambao ni Godwin Simba, Wilson Mshuda, Masanja Madoshi, Seni Silanga, Manyangu Shigukulu, Maendeleo Makoye, Sweye Makungu, Sita Mulemo, Wilson Limbo, Silvatus Masanja na Mtemi Ndamo.

   

 • Hamad ajiunga ramsi ADC

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  HATIMAYE Mbunge aliyemaliza muda wake katika Jimbo la Wawi, Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Bw. Hamad Rashid Mohamed, jana umejiunga rasmi na Chama cha Allience for Democract Change (ADC).

  Baada ya kumpokea Bw. Mohamed, Dar es Salaam jana, chama hicho kilimkabidhi kadi namba moja ya uanachama na kummwagia sifa lukuki akidaiwa ni miongoni mwa viongozi wachache waadilifu na wenye
  uzalendo kwa Taifa lao.

  Akizungumza katika utambulisho huo, Mwenyekiti wa ADC Taifa, Bw. Saidi Miraji, alisema Bw. Mohamed alikuwa mlezi wa chama hicho, mshauri na alihusika kwa namna moja au nyingine kutoa wazo la kuanzishwa ADC.

  Alisema katika kipindi hicho, mwanasiasa huyo alikuwa anakishauri kwa karibu chama hicho katika harakati zake hivyo wanamshukuru kwa mchango wake ambao umesaidia kukifikisha hapo kilipo.

  Kuelekea Uchaguzi Mkuu

  Bw. Miraji alimuomba Rais Jakaya Kikwete wakati huu ambao anakaribia kuondoka madarakani, ahakikishe anakutana na viongozi wa vyama vya upinzani ili kuzungumzia mchakato wa uchaguzi mkuu.

  Alisema wamesikia na kumuona Rais Kikwete akipita kuaga katika maeneo mbalimbali nje na ndani ya nchi hivyo kuna kila sababu ya rais kukutana ili kuagana na viongozi wenzake wa vyama vya siasa nchini kwani huo ndiyo ustaarabu.

  "Kuna mengi ya kuzungumza naye ili kupeana mawazo, ADC ni chama chenye hamu ya kuona Tanzania ina viongozi wenye utamaduni wa uvumilivu kisiasa na kimaisha ili kulijenga Taifa letu," alisema.

  Kwa upande wake, Bw. Mohamed alisema amefurahi kujiunga na chama hicho ambacho kina sera zenye mtazamo wa tofauti na vyama vingine na kumtanguliza Mungu ili kupambana na maovu kama rushwa, vita dhidi ya dawa za kulevya, ujangili na vitendo vingine viovu.

  Alisema yeye binafsi hajahama CUF bali alifukuzwa uanachama baada ya kuonekana anatetea ujenzi wa demokrasia ndani ya chama kwa kutaka kugombea uongozi na kutaka makubaliano ya CUF na CCM yatekelezwe.

  Alitangaza nia yake ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa tiketi ya ADC akiwataka wanachama wengine wajitokeze kuwania nafasi hiyo kwa upande wa Bara na Zanzibar.

 • Baraza kumuhoji Chenge Julai 28

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  BARAZA la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, linatarajia kumuhoji Mbunge wa Bariadi Magharibi, mkoani Simiyu, anayemaliza muda wake, Bw. Andrew Chenge kuhusu tuhuma ya kujipatia mgawo wa fedha kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

  Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na baraza hilo Dar es Salaam jana, ilisema Bw. Chenge anatarajiwa kuhojiwa rasmi Julai 28, mwaka huu na baadaye atahojiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw. Philip Saliboko.

  Awali baraza hilo lilikubali ombi la Bw. Chenge ambaye alikata rufaa Mahakaa Kuu akipinga kuhojiwa lakini ombi hilo lilitupwa ambapo awali mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji mstaafu Balozi Khamisi Msumi, alisema wao hawana kipingamizi juu ya mbunge huyo kukata rufaa dhidi ya shtaka lililokuwa linamkabili.

  "Haijawahi kutokea kwa mtu aliyeitwa kuhojiwa na baraza halafu akate rufaa...maamuzi ya Mahakama Kuu yatasaidia zaidi," alisema.

  Kwa mujibu wa hati ya malalamiko iliyosomwa na Mwanasheria wa Sekretarieti hiyo, Hassan Mayunga, alisema Bw. Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.

  "Mlalamikiwa baada ya kustaafu katika nafasi hiyo Desemba 24,2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL," alisema Bw. Mayunga.

  Alisema kitendo cha mlalamikiwa kuingia mkataba na VIP ni ukiukwaji wa fungu la 6 (j) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha na utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata alipokuwa anatekeleza majukumu yake binafsi.

  "Kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa VIP akiwa na wadhifa wa ubunge ni ukiukwaji wa fungu la 6(e) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa kimaslahi," alisema.

  Aliongeza kuwa, mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na kampuni ya VIP ulimpatia manufaa ya kifedha ya sh. bilioni 1.6 kinyume na fungu la 12(1)(e) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

  Bw. Mayunga alidai mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyonayo katika mkataba wa TANESCO na IPTL kinyume na fungu la 14 la Sheria ya Maadili wala hakutamka madeni aliyokuwa akiidai VIP kwa Kamishna wa Maadili kinyume na matakwa ya fungu la 9(6)(b) la sheria hiyo.

  Mkurugenzi Tabora ahojiwa

  Jana baraza hilo lilimuhoji aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Sipora Liana ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tabora.

  Kwa mujibu wa Mwanasheria wa bazara hilo, Bw. Mayunga alisema shauri hilo namba tatu la mwaka 2013, lilianza kusikilizwa awali na sasa ni muda wa mshtakiwa kupeleka mashahidi wake.

  Liana alishtakiwa katika baraza hilo akidaiwa kukiuka Sheria namba 12(C) cha Maadili ya Umma kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mkuranga, Dkt.Francis Malya lakini alikana shtaka hilo na kuliomba baraza limruhusu kupeleka mashahidi wengine.

  Akizungumza mbele ya Baraza hilo Dar es Salaam jana, Liana alisema si kweli kwamba alimsimamisha kazi ofisa huyo kwani alikuwa akipokea mshahara na kufika ofisini isipokuwa alikuwa hafanyi baadhi ya kazi.

  "Nina mashahidi wanne akiwemo Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Hajjati Amina Said Mrisho, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambaye alikagua hesabu za Halmashauri na kuamuru wafanyakazi 69 kulipia upotevu wa fedha za umma.

  "Pia yupo Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Ofisa Manunuzi kutoka Wizara ya Uchukuzi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ambao wote walikuwepo kipindi hicho," alisema.

  Akitoa ushahidi wake kwa baraza hilo, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mkuranga, Damasi Pasalam, alisema baada ya uchunguzi wake aligundua Liana ni mchapakazi na kulikuwa na makundi yaliyoundwa na baadhi ya watendaji katika halmashauri ili walinde maslahi yao.

  Alisema kulikuwa na ukiukwaji wa mzabuni aliyesababisha wakulima kushindwa kuvuna mazao yao kutokana na ofisa kilimo wa wakati huo kufanya mazungumzo binafsi badala ya kufuata taratibu za kisheria.

  Aliongeza kuwa, pia kulikuwa na miradi hewa mingi ikiwemo ya uchimbaji visima na mabwawa ambayo hadi leo hayatoi maji hivyo Liana aliamua kufuatilia miradi yote na alipobaini upotevu huo, alianza kufuata sheria na hapo akaanza kuchukiwa na baadhi ya maofisa kwa kushirikiana na madiwani hivyo kutengeneza makundi ili kulinda maslahi yao.

  Alisema kulikuwa na mashamba darasa hewa hivyo hadi sasa baadhi ya waliohusika majalada yao yapo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

 • BVR Dar vurugu tupu, RC afafanua dosari zake

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  UANDIKISHWAJI wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR, jijini Dar es Salaam, umeendelea kukumbwa na dosari mbalimbali baada ya wananchi katika baadhi ya vituo kufanya vurugu, kutishia kuwapiga wasimamizi na kuharibu mashine zinazotumika kuandikisha.

  Idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kwenye vituo vya uandikishaji kuanzia alfajiri lakini baadhi yao walijikuta wakishindwa kuandikishwa kutokana na mashine kushindwa kufanyakazi na kusababisha vurugu.

  Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya vituo, uliwakuta wananchi wengi kwenye foleni wakiendelea kuandikishwa na wengine wakisubiri mashine zilizoshindwa kufanyakazi zitengenezwe waweze kuandikishwa bila kujua zitapona saa ngapi.

  Katika vituo vingi, wananchi walionekana kuwa na jazba kutokana na kukaa muda mrefu vituoni bila kupata huduma na wengine wakidai kufika vituoni humo tangu usiku wa manane.

  Katika Kituo kilichopo Kata ya Kilakala, wananchi walianzisha vurugu na kutaka kumpiga msimamizi wakidai kuchoshwa na mashine hizo kutofanyakazi na kumtaka aondoke eneo hilo na mashine husika kwani hazikuwa na uwezo wa kuandikisha wananchi.

  Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema wananchi zaidi ya 500 waliamua kuondoka kituoni hapo baada ya mashine kushindwa kufanyakazi.

  Msimamizi ambaye alinusurika kupigwa katika kata hiyo, Bw. Peter Makoye, alisema hata yeye asingeweza kutatua tatizo hilo kwani fundi wa mashine hizo yuko mmoja kwa vituo vyote vya kata nzima.

  Katika Kata ya Yombo Vituka, uandikishaji uligubikwa na utata mwingi kutokana na wananchi kushindwa kuandikishwa katika vituo vingi kutokana na mashine kushindwa kufanya kazi na baadhi ya vituo zikishindwa kuwaka kabisa kutokana na kukosekana umeme.

  Wananchi walikuwa wamerundikana kwenye vituo wakiwa kwenye makundi kila mmoja akilalamika na wengine wakiwalalamikia waandikishaji kupenyeza wanaowafahamu na ugeni walionao katika matumizi ya mashine.

  Kituo cha Chalinze Mzambarauni na Machimbo, watu wengi waliamua kuondoka baada ya uandikishaji kufanyika kwa kusuasua.

  Katika Kata ya Ukonga, uandikishwaji ulikumbwa na sintofahamu ambapo katika baadhi ya vituo wananchi walianzisha vurugu kwa madai ya kubadilishiwa mfumo wa uandikishwaji kwa maana ya kupewa namba lakini jana walitakiwa kupanga foleni jambo ambalo walilipinga.

  Vurugu pia zilitokea kwenye Vituo vya Mazizini na Mazizini QT baada ya wananchi kufanya fujo na kutishia kuziharibu mashine ambazo zilishindwa kufanyakazi.

  Tamko la RC Dar es Salaam

  Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Saidi Mecky Sadiki, alisema Serikali imeanza kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kuagiza vifaa vingine ili viweze kutumika katika uandikishaji wapigakura.

  Bw. Sadiki, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya vituo na kusema baadhi ya dosari hizo zimechangiwa na mashine ambazo jana zimeanza kusambazwa nyingine katika vituo hasa Wilaya ya Kinondoni.

  Aliwataka watumishi walioteuliwa na kupewa mafunzo kwa ajili ya kusimamia uandikishaji huo, wafike mapema kwenye vituo na kuwaagiza Maofisa Watendaji, kusimamia uandikishaji huu bila kuharibu utaratibu.

  Aliwapiga marufuku wafuasi wa vyama vya siasa wanaofika katika vituo hivyo wakiwa na sare za vyama vyao kwani huo si utaratibu hivyo wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

  Mchakato wa kuandikisha wapigakura jijini humo ulianza juzi ambapo katika baadhi ya maeneo, mashine ziligoma kusoma vituo husika.

   

kimataifa

UN yalaumiwa kutotatua mzozo Yemen

Friday, July 24 2015, 0 : 0


MKUU wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen, Muhammad Ali al-Houthi amezungumzia kuhusiana na kushindwa kwa juhudi za umoja wa mataifa katika kumaliza machafuko na mashambulio yanayofanywa na Saudia nchini humo.

Al-Houthi amesema hayo wakati alipokutana na mratibu wa masuala ya kibinadamu wa umoja wa mataifa nchini Yemen Johannes Van-Der-Klaauw, ambapo pia waliweza kujadili jinsi Saudia walivyoteka maeneo mengi nchini humo.

Hujuma zinazofanywa na Saudia dhidi ya Yemen ni pamoja na milipuko ya angani inayofanywa na Saudia ambapo ndege za utawala huo zimekuwa zikilenga kila kitu kilichoko juu ya ardhi ya Yemen zikiwemo, shule, hospitali pamoja na ofisi za misaada ya kibinadamu.

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen amesisitiza kuwa, mapigano hayo yanakiuka waziwazi mikataba ya kimataifa ikiwemo haki za kuwalinda watoto na wanawake vitani.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, amesema kuwa mpango wa ugawaji misaada ya kibinadamu nchini humo bado unaendelea na pia umoja huo bado unaendelea na juhudi za kuokoa maeneo yote yaliyozingirwa na Saudia.

Wakati huo huo, maelfu ya vijana wa Yemen wamejiunga na harakati ya wananchi ya Answarullah ili kupambana na makundi ya kigaidi ya al Qaida na Dola la kiislam katika maeneo ya Aden huko kusini magharibi mwa Yemen na Taiz.

Kwa mujibu wa habari hiyo, kanali kadhaa za lugha ya Kiarabu katika siku za hivi karibuni zimeamua kufanya kazi kwa uratibu wa pamoja wa kueneza propaganda za kuwavunja moyo wananchi na askari wa Yemen kwa kudai kuwa, eti mji wa Aden umetekwa na vibaraka wa Saudi Arabia.

Mkuu wa harakati ya wananchi ya Answarullah, Abdul Malik al Houthi, amekanusha uvumi huo na kuvitaka vikosi vya wananchi vya nchi hiyo kuelekea huko Aden kwenda kuwasaidia wananchi wa mji huo kupambana na magaidi wa al Qaida.

 

Burundi: 2 wauawa, kura zahesabiwa, Marekani watoa neno

Thursday, July 23 2015, 0 : 0


WATU wawili wameripotiwa kuuawa katika vurugu katika uchaguzi wa Rais nchini Burundi uliofanyika juzi.

Sauti za milipuko na ufyatuaji risasi zilisikika katika mji wa Bujumbura wakati wa kufanyika zoezi la upigaji kura hapo juzi.

Taarifa kutoka nchini Burundi zinasema kuwa shughuli ya kuhesabu kura imeanza hapo jana kufuatia uchaguzi wa urais ambao umetiliwa shaka na watu wengi nchini humo na hata kimataifa.

Rais Pierre Nkurunziza anatarajiwa kupata ushindi mkubwa kwa muhula wa tatu ambapo upinzani umesusia kabisa kura hiyo.

Huku hayo yakijiri Marekani na Uingereza wamekashifu kura hiyo wakisema kuwa haikuwa ya huru na haki.

Marekani kwa upande wake imependekeza kugawana madaraka huku ikitishia kuchukua hatua dhidi ya Burundi iwapo mwafaka hautapatikana.

Uchaguzi huo wa Rais nchini Burundi ulifanyika juzi licha ya malalamiko ya wapinzani na hata hatua yao ya kususia uchaguzi huo nayo haikusaidia.

Aidha malalamiko ya jamii ya kimataifa na hata miito ya kutaka kuahirishwa uchaguzi huo nayo haikuweza kubadilisha serikali ya Burundi juu ya kuahirisha uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umefanyika huku wapinzani wakisisitiza kwamba kufanyika kwa uchaguzi huo kutazidi kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa na kuzifanya juhudi za kuutafutia ufumbuzi kukwama.

Asasi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Afrika hazijatuma waangalizi wake katika uchaguzi wa Burundi zikisisitiza kwamba hakukuwa na mazingira ya kufanyika uchaguzi huo katika anga ya uhuru na haki na hivyo kuufanya uchaguzi huo kutokuwa wa halali.

Wapinzani wanapinga hatua ya Nkurunziza kugombea urais kwa mara ya tatu wakisema inaenda kinyume cha katiba na mapatano ya amani ya mwaka 2006 ya mjini Arusha, Tanzania.

Watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha tokea mwezi Aprili wakati wapinzani walipoanza maandamano dhidi ya serikali.

 

 

 • Kambi ya al-Shabaab yadhibitiwa na jeshi

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  VIONGOZI wa serikali ya Somalia wametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kudhibiti ngome ya kundi la wapiganaji la Al-Shabaab nchini humo.

  Jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya kusimamia amani nchini Somalia AMISOM walitekeleza operesheni kali katika mji wa Bardher, kusini mwa Somalia na kufanikiwa kudhibiti ngome hiyo muhimu.

  Aidha watu walioshuhudia wamesema kuwa mapigano makali yametokeo katika maeneo ya kando na mji huo wa Bardher baina ya majeshi ya serikali kwa kushirikiana na askari wa AMISOM na wapiganaji wa al-Shabaab.

  Kamanda mmoja wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binadamu, anayeitwa Shekhe Ahmad Abu Ubaidah, sanjari na kuthibitisha habari ya kupoteza kambi hiyo muhimu amedai kuwa wanachama wa kundi hilo hawajashindwa na kwamba bado wanaendeleza mashambulizi.

  Hivi karibuni kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kiliahidi kuwafurusha wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi kutoka vijiji na miji ya kusini mwa nchi hiyo.

  Aidha AMISOM ilitangaza habari ya kuanzishwa operesheni kali kwa jina la 'Juba Coridor' kwa ushirikiano wa jeshi la Somalia lengo likiwa ni kuyadhibiti maeneo muhimu kama Bay na Gedo yanayopatikana kusini mwa Mogadishu.

 • Uganda yampandisha kizimbani kiongozi wa waasi wa ADF

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  KIONGOZI wa kundi la waasi wa ADF la nchini Uganda, Jamil Mukulu amepandishwa kizimbani katika mahakama ya nchi hiyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

  Hatua hiyo imechukuliwa wiki chache baada ya kiongozi huyo kukabidhiwa kwa serikali ya Uganda.

  Kwa mujibu wa Fred Ananga, Msemaji wa Polisi ya Uganda, Jamil Mukulu alipandishwa kizimbani juzi Jumatano na kusomewa mashtaka ya kutenda jinai dhidi ya binadamu na uhaini dhidi ya nchi yake ya Uganda.

  Ananga ameongeza kuwa ulinzi uliimarishwa wakati wa kikao cha kesi ya Jamil Mukulu katika mkoa wa Jinja ulio umbali wa kilometa 85 mashariki mwa jiji la Kampala.

  Mukulu alitiwa mbaroni na maafisa usalama nchini Tanzania na kukabidhiwa kwa serikali ya Uganda.

  Waasi wa ADF walianzisha harakati ya uasi dhidi ya Rais Yoweri Museven wa Uganda kuanzia mwaka 1990 na baada ya hapo walipiga kambi katika maeneo yaliyo mpakani baina ya Kongo DRC na Uganda.

  Katika kipindi hicho waasi hao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo yamekuwa yakiambatana na utekaji nyara watoto na kuendesha biashara haramu katika maeneo hayo.

  Hivi karibuni wakazi wa maeneo ya Beni kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia, waliitaka serikali ya Uganda kumkabidhi Jamil Mukulu kwa serikali ya mji huo wa Beni kwa lengo la kuhukumiwa katika eneo alikotenda jinai hizo.

   

 • Buhari: Marekani inawasaidia Boko Haram!

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  RAIS wa Nigeria, Mahammadu Buhari ameishutumu Marekani kuwa inawasaidia na kuchochea kundi la wanamgambo wa Boko Haram kufanya machafuko nchini Nigeria pamoja na katika nchi jirani kwa kukataa kutoa silaha kwa Nigeria.

  Sheria ya Marekani inazuia serikali kuuza silaha kwa nchi ambazo zinashindwa kushughulikia ipasavyo masuala ya haki za binadamu.

  Kundi hilo la Boko Haram linatajwa kuwateka wasichana na wanawake wengi wakiwemo wasichana wa shule zaidi ya 200.

  Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alikutana na rais Barack Obama Jumatatu kuomba msaada zaidi.

  Kundi la Boko Haram limewauwa watu 10,000 tangu mwaka 2009 na limewateka mamia ya wasichana na wanawake.

   

 • DRC: Tumeongeza hujuma dhidi ya waasi wa kihutu

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  JESHI la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeongeza mashambulizi dhidi ya waasi wa nchini Congo.

  Lambert Mende Omalanga, Msemaji wa Serikali ya Congo amesema kuwa mashambulizi ya jeshi la serikali yameongezeka dhidi ya ngome za waasi wa kihutu katika maeneo tofauti, hususan Kivu Kaskazini na Kivu Kusini pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Katanga.

  Lambert ameongeza kuwa mbali na kuwatia mbaroni waasi kadhaa tangu mwanzoni mwa operesheni hiyo, wapiganaji wanne wa waasi hao wanaopigana kwa lengo la kuikomboa Rwanda huko mkoani Kivu Kaskazini, wameuawa.

  Zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha kutokana na machafuko ambayo yamekuwa yakijiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

biashara na uchumi

Waishukuru Airtel kwa kuwajengea mnara

Friday, July 24 2015, 0 : 0

WAKAZI wa Kijiji cha Kigwang'oko Wilaya ya Ulyankulu, wameipongeza kampuni ya Airtel kwa kuwajengea mnara wa mawasiliano na hivyo kuondokana na tatizo sugu la mawasiliano lililokuwa likiwakabili.

Wakazi hao wamekuwa wakifanya shughuli zao bila ya mawasiliano ya uhakika kwa muda mrefu jambo linalotajwa kukwamisha shughuli nyingi za maendeleo kijijini hapo.

Wanakijiji hao wameeleza kuwa, wamekuwa wakipata tabu ya kufanya mawasiliano wakati mwingine wakilazimika kupanda kwenye miti au vichuguu kupata mawasiliano kabla ya kujengwa kwa mnara huo.

"Tunawashukuru sana Airtel kwa kutukumbuka na kutuletea mnara huu ambao hapa kijijini kwetu ni mkombozi mkubwa katika sekta ya mawasiliano," alisema mmoja wa wakazi hao Juma Magema.

"Kabla ya Airtel kuweka mnara hapa kijijini kwetu tulikuwa tunapanda katika miti na hata vichuguu ili kupata mawasiliano, lakini sasa hatupati tena shida hiyo,"alisema.

Akizindua mnara huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, John Kadutu, amewataka wananchi kuutumia mnara kuboresha shughuli zao za kijamii na kiuchumi na kuboresha maendeleo ya kijijini hapo na jamii kwa ujumla.

"Muutumie mnara huu kujiletea maendeleo kwani hivi sasa mnaweza kutumia mawasiliano ya Airtel na huduma zote zinazoenda sambamba na uwepo wa mnara huo kijijini hapo," alisema Kadutu.

Awali meneja wa Airtel Mkoa wa Tabora, Fidelis Lugangira, alisema wamepeleka mnara huo ili kuboresha kiuchumi, lengo likiwa ni kuzidi kuwafanya wanufaike kwa kutumia mawasiliano.

"Mnara huu umejengwa kijijini hapa ikiwa ni hatua ya kampuni yetu kusogeza karibu huduma za mawasiliano hivyo ni fursa ya kipekee kwenye kujiletea maendeleo," alisema Lugakingira.

Airtel imezindua huduma ya mawasiliano katika Kijiji cha Kigwang'oko Wilayani Ulyankulu mikoani Tabora mara baada ya kuzindua huduma kama hizo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida na katika kijiji cha Nduruma wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Mpango mkakati ni kufikia maeneo mengi zaidi hususani yaliyoko pembezoni mwa nchi.

Airtel yatangaza washindi 'Jiongeze na Mshiko'

Thursday, July 23 2015, 0 : 0


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel imechezesha droo ya kwanza ya promosheni ya 'Jiongeze na Mshiko' na kutangaza washindi wawili wa kwanza wa wiki waliojishindia kila mmoja pesa taslimu.

Akizungumza kuhusu droo ya promosheni hiyo Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema Promosheni ya "Jiongeze na Mshiko" itawawezesha Watanzania kujiunga na kushiriki bure na kupata nafasi ya kujishindia sh. milioni moja kila wiki na mwisho wa promosheni kujishindia sh.milioni mbili.

Lakini mteja anaweza kuamua kujiongeza na kushiriki kwa tozo ya shilingi 300 kwa siku na kupata nafasi ya kujishindia zawadi nono zaidi ikiwa ni pesa taslimu sh. milioni 3 kila wiki na mwisho wa promosheni atashinda sh.milioni 50.

Akitangaza washindi Mbando alisema;" Leo tumechezesha droo ya wiki ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa promosheni ya "Jiongeze na Mshiko" wiki iliyopita.

"Ninayo furaha kutangaza washindi ambao ni pamoja na Plasikus Gabriel Balimasu (25), mlinzi na mkazi wa Mkoa wa Geita yeye amejishindi sh. milioni 3 na mshindi wa pili ni Rashidi Hassan Mshabaha (27), mfanyabiashara ndogondogo na mkazi wa mkoa wa Mtwara yeye amejishindi sh.milioni 1.

"Tunaamini ushindi huu utawawezesha wateja wetu kupata fedha za kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha yao, hilo ndilo lengo letu kama Airtel kupitia kampeni yetu.

 • Watumishi watakiwa kutoogopa mikopo

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  WATUMISHI wa Serikali na Taasisi nchini wametakiwa kutokuogopa kuchukua mikopo katika mashirika yanayoshughulika na kazi hiyo.

  Akizungumza na Majira, Meneja wa Faidika mkoani Dodoma, Emanuel Lumbumbu alisema watumishi wengi wamekuwa na uoga katika kuchukua mikopo na kudai kuwa wengi wamekuwa wakiona kama mkopo ni mzigo.

  Lumbumbu alisema kuwa taasisi ya FAIDIKA imekuwa ikitoa mikopo kwa watumishi wa Serikali na mashirika zaidi ya elfu moja kwa mwaka na kuongeza kuwa mikopo hiyo imekuwa ni msaada mzuri kwa watumishi hao kujikwamua kiuchumi.

  "FAIDIKA inatoa mikopo pamoja na elimu kwa wateja wake lakini sasa wengi wamejenga dhana ya kusema kuwa mikopo ni mzigo pia ni kero, tunawatoa hofu mikopo si mzigo na imekuwa ikisaidia sana jamii katika mambo mbalimbali,"alisema Lumbumbu.

  Aidha Bw.Lumbumbu alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyakazi wa Serikali hususani wenye kima cha chini cha mshahara ili iweze kuwainua kiuchumi.

  "Tuliona tutoe mikopo kwa wafanyakazi wenye mishahara midogo na hata wale wenye mishahara ya juu lengo kubwa ikiwa ni kuwainua kiuchumi, unaweza kuchukua mkopo ukaanzisha mradi wowote hata kujenga nyumba na mambo mengine ambayo ungefanya kwa kutegemea mshahara pekee isingewezekana.

  Alisema kwa kuanzisha taasisi hiyo wameweza kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza ofisi katika maeneo ambayo hawakuwa na ofisi kipindi cha awali.

 • Wanawake watakiwa kujiunga kwenye vikundi

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Tarime Mkoani Mara wametakiwa kujiunga katika vikundi ili Serikali iweze kuwapatia mikopo na kujikwamua kimaisha kwa kuanzisha biashara.

  Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Uchumi wa wilaya ya Tarime Mkoani Mara John Gimunta kwenye semina ya UWT ya wajasiriamali ambayo iliandaliwa na mwenyekiti wa umoja huo Paulina Monanka kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake ili kujikomboa kutoka katika wimbi la umaskini.

  Gimunta alisema kuwa Serikali haina hela ya kugawia na kumpa kila mtu mmoja mmoja isipokuwa kama watu watajikusanya pamoja na kuunda vikundi ambavyo vinatambulika kisheria serikali itawasaidia na kuwapa mikopo.

  Aidha Gimunta aliwataka wanawake hao kujifunza kuwa na tabia ya kurejesha mikopo pindi wanapokopeshwa ili kuwa rahisi na wengine kupata mikopo.

  Aidha semina hiyo ilienda sambamba na kuelimisha wanawake wa umoja huo juu ya ujenzi wa jumuia ya wanawake kuwa ni chombo muhimu, maadili ya uongozi.

  Katika semina hiyo wanawake walitaka kujua ni namna gani viongozi wanawasaidia wapiga kura katika maeneo yao punde wanapopatwa na matatizo.

  Akijibu hoja hiyo mwezeshaji Maxmiliani Ngesi ambaye ni Katibu Mwenezi na Itikadi na pia ni mwandishi wa habari wa Redio Free Afrika alisema kuwa viongozi wazembe ambao hawawajibiki ipasavyo kwa wananchi ambao waliwachagua nafasi hiyo inawapa mwanya viongozi wa chama cha upinzani kupata nafasi ya kuisema CCM,

  Aidha Ngesi aliwataka viongozi kuwajibika katika maeneo yao kwa wananchi waliowachagua kwa kuwa walikuwa na imani kuwa watawasaidia punde watakapoingia madarakani.

  Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya Tarime Paulina Monanka aliwashukuru wawezeshaji hao kwa kuitikia wito pamoja na mgeni rasmi kukubali kufadhili semina hiyo sanjari na kukubali kufungua semina na kuwapa elimu wanachama.

 • Wabunge Afrika Mashariki wapongezwa kwa maendeleo

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  KATIBU wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bw. Yahya Khamis Hamad, amesema kuwa kwa kiasi kikubwa mabunge ya Afrika yamepiga hatua za kimaendeleo kutokana na kuwapo kwa ushirikiano mzuri wa makatibu wa nchi hizo.

  Katibu huyo aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mpango mkakati wa Jumuiya ya Makatibu Wakuu (SOCATT) wa nchi 19, uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Z-Hotel, iliyopo Kihinani Mkoa wa Mjini Unguja.

  Alisema ni wazi kuwa tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo mabunge mengi yameweza kupata maelewano mazuri, pamoja na kutambua na kuzifanyia kazi changamoto zilizokuwa zikiwakabili kipindi cha nyuma.

  Alisema njia kuu iliyofanikisha kwa mabunge ya nchi hizo ni kubadilishana mawazo ya kiutendaji mara kwa mara, jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa kushirikisha makatibu mezani wa mabunge hayo.

  "Kiukweli mabunge ya Afrika yameweza kupiga hatua za kimaendeleo kutokana na kuwapo kwa ushirikiano mwema kati ya makatibu sisi kufuatia kuwapo kwa Jumuiya yetu hii ya nchi 19 za Afrika,"alisema.

  Hata hivyo alisema kuwa jambo jingine ambalo limewawezesha kupiga maendeleo kwa kiasi kikubwa kwa mabunge hayo ni pale pindi bunge moja likiwa na tatizo basi tatizo hilo huchukuliwa kama ni la mabunge yote.

  Jambo ambalo alisema kuwa huwa linapatiwa ufumbuzi wa kitaalam kwa kuwashirikisha wajumbe wote, huku kila mmoja akitoa mchango wake wa kutatua tatizo lililolitapa bunge husika.

  Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar katibu huyo alisema wameweza kupiga hatua kwa kasi kutokana na kuwapo kwa ushirikiano mwema kwa wajumbe wote wa baraza hilo katika vikao vyao.

  Bw.Yahya alizidi kufahamisha kuwa kabla ya kuwapo kwa serikali ya umoja wa kitaifa baraza la wawakilishi lilikuwa haliende vyema kutokana na wajumbe hao kutokuwa na umoja, huku kila upande ukishambulia upande wa mwenzake kisiasa.

  Naye mwenyekiti wa mkutano huo Bw. Eric Phindera, kutoka nchini Afrika ya Kusini alisema kwa kiasi kikubwa mabunge ya nchi za Afrika hasa yaliyounda umoja huo yameweza kufaidika katika masuala ya kidemokrasia.

  Alisema kuwa hali hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa ushirikiano wa kila hali kwa makatibu wakuu wa nchi hizo kwa pamoja kutoa ushirikiano wao kwa Bunge la nchi yoyote pindi likitokewa na tatizo la aina yoyote.

 • 'Mitandao ya kijamii ipanue wigo wa uzalishaji, masoko'

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  WATANZANIA wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kupata taarifa mbalimbali na kuzitumia katika maendeleo.

  Ushauri huo umetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Utendaji ya Kituo cha Ushirikiano wa kilimo na Maendeleo Vijijini cha nchi za Umoja wa Ulaya, Afrika, Karebiani na Pasifiki (CTA), Profesa Faustin Kamuzora.

  Alisema taarifa hizo zina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za kilimo, usindikaji, biashara na ukuzaji wa masoko katika ukanda wa Afrika Mashariki na Dunia nzima kwa ujumla.

  Akifungua mafunzo ya mawasiliano ya mitandao ya kijamii jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna kila sababu kwa Watanzania kutumia mitandao hiyo kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara.

  ìMitandao hii imekuja kutuongezea tija...inaokoa muda. Ikitumika vyema ina faida kubwa,î alisema Kamuzora ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe anayeshughulikia Utawala na Fedha.

  CTA na Baraza la Nafaka la Afrika ya Mashariki (EAGC) wanashirikiana kutoa mafunzo kwa wajumbe kutoka taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya mitandao ya kijamii.

  Aliwataka wanasemina hao kupitia ujuzi watakaoupata kuusambaza katika taasisi zao na kuwa tayari kuwapa wananchi taarifa juu ya hali ya hewa, masoko na bei ya mazao ya nafaka, na mifugo kupitia mitandao kama blogs, facebook na Twitter.

  Pia aliwataka wanapotumia mitandao hiyo wakumbuke kufuata sheria inayoongoza katika sekta hiyo ndogo.

  Kwa upande wake, Meneja Miradi wa EAGC, Bw. Ikunda Terry alisema baraza lao limeamua kuandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na CTA kuwaleta wadau mbalimbali wanaojihusisha na teknolojia hii kuwafundisha namna ya kupeleka ujumbe na elimu kwa jamii.

  ìKwa sasa watu wengi wanatumia mitandao hii ya facebook, twitter na simu za mkononi kufanya kazi kwa kuwa ni njia nyepesi kufikisha ujumbe kwa haraka, kwa watu wengi na mbali,î Terry alisema.

  Ofisa Mipango wa EAGC, Gidion Murenga, alisema Afrika Mashariki inajitosheleza kwa mazao ya chakula lakini kuna shida ya kisera katika kuhakikisha biashara inafanyika.

  ìBaraza hili linahamasisha biashara ya mazao ya nafaka, tunataka wadau wajifunze mbinu za kutoa taarifa nzuri zinazosaidia kukuza biashara ya mazao hayo,î alisema.

  Wajumbe 30 kutoka taasisi mbalimbali nchini wananufaika na mafunzo hayo ya wiki nzima.

michezo na burudani

Ni Yanga na KMKM leo Taifa

Friday, July 24 2015, 0 : 0

MABINGWA wa Tanzania Bara Yanga wanashuka uwanjani leo kuvaana na mabingwa wa Zanzibar KMKM kutafuta nafasi ya kucheza Robo Fainali katika michuano ya Kombe la Kagame.

Yanga watakuwa na kibarua cha kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu, ili kujiweka katika mazingira mazuri na uhakika wa kupita huku KMKM nao wakiwa wanataka kuondoka na ushindi.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema kwa sasa macho yao yote yapo katika mechi dhidi ya KMKM kwani ni moja ya mechi muhimu sana kwao.

Alisema hawezi kuongelea mchezo uliopita kwani kwa ushindi walioupata ana imani wembe utakuwa ni huo huo tu.

Mkwasa alisema kuna makosa madogo madogo ya kimchezo na hilo wameliona, kwani hata katika mechi iliyopita wachezaji waliingia kwa presha kubwa ya kutaka goli la mapema.

"Wachezaji waliingia na presha kubwa ya kutaka goli la mapema na hilo likafanya tuweze kukosa nafasi nyingi sana za wazi ikiwemo na penalti mbili", alisema Mkwasa.

Kuhusu kukosa kwa penalti kwa wachezaji wake wawili Simon Msuva na Amisi Tambwe, alisema ule ni mchezo na siku zote penalti haina ufundi hata hivyo mazoezini wachezaji wote wanapiga penalti vizuri ila ukija uwanjani kuna kuwa na msukumo zaidi wa mashabiki.

Yanga ilifanikiwa kuifunga timu ya Telecom mabao 3-0, ambayo tayari imeshaaga mashindano hayo kwa kufungwa mechi zote tatu walizocheza.

Huu utakuwa ni mchezo wa tatu kwa Yanga ambao wanatakiwa kushinda dhidi ya KMKM wenye pointi sawa ila tofauti kwa mechi walizocheza.

KMKM watakuwa wanatupa karata yao ya mwisho, ambapo wakifungwa watakuwa wamefungasha virago na kurejea visiwani Zanzibar.

Kocha Mkuu wa KMKM, Ali Bushiri bado hajakata tamaa ingawa uwezekano wa kupita ni mdogo kwani ni mojawapo ya kundi gumu ikizingatiwa timu zinazoongoza zina pointi nyingi na mchezo mmoja mkononi.

Iwapo KMKM watashinda mchezo huo watakuwa wanamuombea vibaya Yanga afungwe mechi yake dhidi ya Khartoum siku ya Jumapili.

Nayo timu ya Gor Mahia wanatarajia kukutana na Khartoum wote wakiwa na pointi sawa, ila tofauti ya magoli.

Timu hizo zinakutana huku kila moja ikiwa imecheza mechi tatu.

Katika mechi hiyo timu itakayoshinda itakuwa imejihakikishia kuingia hatua ya robo fainali hata kama mchezo wa mwisho atafungwa.

Mechi ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum inatarajiwa kuchezwa saa 8 mchana, huku KMKM dhidi ya Yanga itakuwa ni saa 10 jioni.

 

Yanga SC yainyoosha Telecom 3-0

Thursday, July 23 2015, 0 : 0


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Kagame, Yanga SC jana imezinduka na kuinyuka Telecom ya Djibout mabao 3-0 kwenye mechi ya Kundi A iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mpira ulianza kwa Yanga kupeleka mashambulizi kwa Telecom ambapo dakika ya tatu Haruna Niyonzima aliachia shuti kali lililodakwa na kipa, Nzokira Jeef.

Dakika ya saba, Mousa Ahmed wa Telecom alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini akapiga mkwaju mkali uliopaa juu ya lango la Yanga.

Yanga ilifanya shambulizi lingine tena langoni mwa Telecom ambapo dakika ya nane, Malimi Busungu alipata nafasi nzuri ya kufunga kwa kichwa kutokana na krosi iliyochongwa na Joseph Zuttah lakini mpira ukatoka nje.

Dakika ya 15 Amis Tambwe, aliikosesha Yanga bao baada ya kuachia mkwaju mkali lakini kipa Jeef akapangua mpira na kuwa kona butu.

Tambwe aliikosesha tena Yanga bao baada ya kubaki na kipa Jeef lakini kwa mshangao akapaisha mpira juu ya lango la Telecom.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' alipanda juu kusaidia mashambulizi ambapo dakika ya 20 aliachia shuti lililopaa juu ya lango.

Juhudi za Yanga zilizaa matunda dakika ya 26 baada ya Busungu kuifungia timu hiyo kwa kumchambua kipa akiunganisha pasi ya beki wa timu hiyo raia wa Ghana, Zuttah.

Dakika ya 28 Tambwe na Busungu wakiwa na kipa walishindwa kuifungia bao Yanga baada ya Haji Mwinyi, kumiminika krosi safi safi langoni mwa Telecom.

Yanga ilipata penati dakika ya 39 iliyotolewa na mwamuzi Issa Kagabo kutokana na Simon Msuva kufanyiwa madhambi eneo la hatari, ambayo hata hivyo Tambwe alishindwa kutumbukiza mpira kimiani baada ya shuti lake kutoka nje.

Dakika ya 45 Yanga ilipata penati nyingine baada ya beki mmoja wa Telecom kuunawa mpira eneo la hatari hata hivyo mkwaju wa Simon Msuva ulipanguliwa na kipa na kuwa kona butu.

Baada ya Msuva na Tambwe kukosa penati Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm aliaonekana kukerwa na wachezaji hao kukosa penati na kuamua kuwatoa na nafasi zao kuchukuliwa na Khpa Sherman na Godfrey Mwashiuya ambapo mabadiliko hayo yaliiongezea nguvu timu hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya shambulizi langoni mwa wapinzani wao lakini Sherman akiwa ndani ya 18 alipokea pande safi kutoka kwa Haruna Niyonzima lakini shuti lake likapaa juu ya lango.

Dakika ya 65, Busungu aliipatia Yanga bao la pili baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa kiungo chipukizi wa timu hiyo Mwashiuya.

Yanga iliongeza bao la tatu dakika ya 72 kupitia kwa Mwashiuya, ambaye aliwatoka mabeki wa Telecom na kuachia mkwaju mkali akiwa nje ya 18 uliopita mtambaa panya na kujaa wavuni.

Telecom ilizinduka dakika ya 74 baada ya kufanya shambulizi kali langoni mwa Yanga ambapo mshambuliaji wake Warsama Hussein akiwa nje ya 18 aliachia mkwaju mkali uliopaa juu ya lango.

Hadi mwamuzi wa mchezo, Issa Kagabo anapuliza kipyenga cha kumaliza mpira Yanga iliondoka kifua mbele kwa mabao 3-0.

Mara baada ya mechi kumalizika kocha Pluijm wa Yanga alisema amesikitishwa na wachezaji wake kukosa penati mara kwa mara kwani hata kwenye mchezo wa ufunguzi walikosa penati kupitia kwa nahodha wake Canavaro.

Alisema amegundua kuna upungufu mkubwa uliojitokeza kwa wachezaji wake na hata katika mchezo wa jana kama asingetumia plani B kipindi cha pili wangetoka na ushindi mwembamba.

Michuano hiyo itaendelea tena leo katika uwanja huo ambapo APR ya Rwanda itachuana na LLB ya Burundi saa 10 jioni. Mchezo wa kwanza wa michuano hiyo utazikutanisha timu ya Heegan FC ya Somalia dhidi ya Al Shandy ya Sudan.

 • Poppe: Bado tunamsoma kipa Gor Mahia

  Friday, July 24 2015, 0 : 0


  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kuwa kipa namba moja wa Gor Mahia ya Kenya, Boniface Oluoch ni mzuri, ila wanatakiwa kumuona kwenye mechi nyingine zaidi.

  Kwa upande wa kipa huyo yeye tayari ameshajinadi katika klabu hiyo ya Msimbazi, ambapo amesema ana mambo matatu yanayomfanya kukubali kuichezea Simba kama watakubaliana kila kitu kwa kuwa ameelezwa ndiyo timu inayomfaa.

  Simba kwa sasa inahaha kutafuta kipa ambaye atakuwa akisaidiana na Ivo Mapunda, baada ya kocha wa makipa Abdul Salim kusema kuwa aliyekuwa kipa msaidizi wa timu hiyo, Peter Manyika bado anatakiwa kuwa na uzoefu.

  Oluoch alionesha uwezo mkubwa katika mchezo dhidi ya Yanga, huku akiokoa penalti ya beki wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Kagame.

  Hans Poppe alisema wamevutiwa na kipa huyo kwani alionesha uwezo mzuri kwenye mechi dhidi ya Yanga lakini hawawezi kumjaji kwa mechi moja au mbili.

  "Kipa wa Gor Mahia ni mzuri lakini hatuwezi kumsajili kwa mechi moja au mbili, bado tunazidi kumwangalia kwa kuwa tunataka kipa mwenye rekodi na uwezo wa kuisaidia timu yetu," alisema Hans Poppe.

  Kuna tetesi kuwa Simba imeshaanza mazungumzo na timu hiyo na kuna uwezekano ikamsajili kipa huyo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kagame.

  Alipotafutwa kipa huyo ambaye anaichezea timu ya Taifa ya Kenya, alisema yupo tayari kucheza Tanzania na timu anayoona inamfaa ni Simba pekee.

  "Nipo tayari kucheza soka la Tanzania na timu ninayoipenda kujiunga ni Simba."

   

 • Coastal kuweka kambi nje ya nchi

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  TIMU ya Coastal Union ya Tanga imepanga kwenda kuweka kambi nje ya Tanzania, kwa ajili ya kujifua vilivyo na maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

  Timu hiyo ambayo kwa sasa bado imeweka kambi jijini Tanga imekuwa ikiendelea kujifua vizuri kwa ajili ya ligi hiyo.

  Akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili jana kwa simu, Msemaji wa Coastal Union, Oscar Assenga alisema kwa sasa wanaendelea kufanya mazoezi madogo madogo, ila wana mpango wa kwenda kuweka kambi nje ya Tanzania hivyo kwa sasa wanaangalia ni wapi waweke kambi hiyo.


  Assenga alisema wakiwa kambini wanatarajia kucheza mechi za kirafiki na timu mbalimbali, kabla ya ligi kuanza.

  ìTunampango wa kuweka kambi nje ya Tanzania, lakini bado tunaangalia ni wapi tutaweka hivyo mambo yakiwa tayari tutasema tunaenda wapi na tutaondoka lini,î alisema Assenga.

  Alisema kikosi chao kipo vizuri na baada ya kusajili wachezaji 13, bado kuna nafasi ziko wazi kwahiyo wataangalia kama kuna uwezekano wa kusajili wachezaji wengine.

   

 • Benteke rasmi Liverpool

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  KLABU ya Liverpool imekamilisha rasmi kumsajili mshambuliaji wa Aston Villa, Christian Benteke kwa kitita cha pauni milioni 32.5 kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

  Benteke alikubali mkataba wa muda mrefu na kuwa mchezaji wa pili kununuliwa kwa gharama kubwa huko England.

  Mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji ameifungia magoli 49 katika mechi 101 alizocheza kwenye timu yake ya zamani ya Aston Villa.

 • Mkwasa afurahia mabao

  Friday, July 24 2015, 0 : 0

  KOCHA wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema amefurahishwa na ushindi wa Yanga, ingawa kwa kiasi kikubwa kuna mambo ya kukera yaliyotokea uwanjani.

  Mkwasa aliye pia kocha msaidizi wa Yanga alisema, ushindi ni ushindi lakini ana imani kubwa timu hiyo itabadilika zaidi katika mchezo ujao.

   

  “Nimefurahishwa na ushindi huu, sasa ni kujipanga kwa mchezo unaofuata,” alisema Mkwasa mara baada ya mchezo dhidi ya Telecom ya Djibout.

   

  Alisema ushindi wowote ni ushindi kwa hiyo kwa sasa macho yao yote yapo katika mchezo dhidi ya KMKM utakaopigwa leo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

   

  Yanga walifanikiwa kuifunga Telecom kwa mabao 3-0 magoli yaliyofungwa na Malimi Busungu aliyefunga mawili na Geofrey Mwashiuya.

  Mechi ya awali Yanga walitoka kapa baada ya kufungwa na Gor Mahia 2-1.