kitaifa

Waziri Mbene ahojiwe-CCM

Monday, August 25 2014, 0 : 0

 

KAMATI ya Siasa mkoani Mbeya, imeagiza kuitwa kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Janeth Mbene ili aweze kuhojiwa akidaiwa kujihusisha na vurugu za kisiasa zinazoendelea katika Wilaya ya Ileje, mkoani humo.

Bi. Mbene ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, anadaiwa kujihusisha na kampeni za kuwania jimbo hilo pamoja na kukigawa chama kwa kusababisha makundi.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoani humo, Bashiru Madodi, aliyasema hayo Mjini Mbeya jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema uamuzi wa kuitwa Bi. Mbene, umefikiwa kwenye vikao vya kamati za siasa vilivyoketi kujadili maadili na nidhamu katika Wilaya hiyo na Momba, kati ya Agosti 22 na 23 mwaka huu.

Alisema Kamati ya Siasa Mkoa pia imechukua uamuzi wa kuivunja Kamati ya Siasa Wilaya ya Ileje na kupendekeza kuvuliwa Uenyekiti Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Hezrone Kibona na kuwapa onyo kali Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohamed Mwala na Katibu wa Baraza la Madiwani, Luciano Mbosa.

Katika taarifa yake, Madodi alisema kamati hiyo pia imewasimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kata ya Majengo Mji mdogo wa Tunduma, Bw. Daniel Mwashiuya, Katibu Kata, Bw. Hemed Steven, Katibu wa Uchumi na Fedha, Zainabu Siyame na Katibu Mwenezi wa Kata, Boniface Mwakasege, wakidaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za chama.

"Viongozi hawa wanadaiwa kutumia vibaya fedha zilizotokana na mapato ya vyumba vya maduka yaliyopo Kata ya Tunduma kabla ya kugawanywa Kata za Chapwa, Tunduma na Majengo...Kamati imeunda timu ya kufuatilia malizote za chama zilizopo katika kata hizi," alisema Bw. Madodi.

Akitoa sababu za kuitwa kwa Bi. Mbene, alisema amekuwa chanzo cha vurugu za kisiasa wilayani humo ambapo baadhi ya viongozi wa chama Wilaya wamekuwa wakikaidi maagizo ya chama Mkoa.

Alisema viongozi wa CCM katika Wilaya hiyo, waliamua kufunga ofisi za chama wakishinikiza apelekwe Katibu mwingine ambapo jitihada za uongozi wa Mwenyekiti na Katibu wa CCM Mkoa kuwaomba wafungue ofisi hizo zilishindikana.

Hata hivyo, Agosti 18 mwaka huu, CCM Mkoa kilimwagiza Kibona aitishe Kamati ya Siasa ya Wilaya ili Kamati ya Siasa Mkoa iende kuwasikiliza lakini alikataa na kusema hakuwa tayari kukutana na Kamati ya Siasa Mkoa.

"Hata baada ya Katibu wa CCM wilayani humo kuagizwa aitishe kikao hicho, Kibona aliwashinikiza wajumbe kutohudhuria kikao," alisema Bw. Madodi.

Ajira Uhamiaji zafutwa rasmi

Friday, August 22 2014, 0 : 0

 

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imezifuta rasmi ajira 200 za nafasi ya Konstebo na Koplo wa Uhamiaji baada ya kupokea ripoti ya Kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za upendeleo katika ajira hizo ikidaiwa baadhi ya walioitwa katika ajira ni watoto wa jamaa, ndugu na Maofisa wa Idara ya Uhamiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, alisema baada ya waombaji wa nafasi hizo kufanyiwa usaili na kuitwa kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira hizo kwa ndugu na jamaa za watumishi wa idara hiyo hivyo Wizara ililazimika kuzisitisha na kuunda kamati ndogo ya watu watano ili iweze kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.

Aliongeza kuwa, kamati hiyo ilipewa siku 10 kuanzia Agosti mosi mwaka huu iwe imekamilisha kazi hiyo ambayo waliifanya kwa muda waliopewa na kutoa matokeo.

"Katika uchunguzi wao, kamati imebaini kuwa, baadhi ya wasailiwa waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa watumishi wa idara hii.

"Baadhi ya waombaji wa nafasi hizi, walikuwa na umri mkubwa zaidi ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya kazi (Konstebo miaka 25 na Koplo miaka 30), lakini walisailiwa na kuitwa kazini," alisema Abdulwakil.

Alisema baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu katika ufaulu hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu ambazo zimetolewa ambapo matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa ya jumla na hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na sita.

Abdulwakil aliongeza kuwa, kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, ajira hizo zimefutwa na zitatangazwa upya ambapomchakato wa ajira utasimamiwa na Wizara hiyo ambapo hatua hiyo pia inahusu ajira 28 zilizokuwa zimetangazwa na kujazwa kwa upande wa Ofisa Uhamiaji Zanzibar.

Aliongeza kuwa, awali ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika gazeti la Serikali Februari 17 mwaka huu na kutoa tangazo hilo kwenye tovuti ya Wizara na Idara ya Uhamiaji.

"Baada ya kutangazwa ajira hizi, maombi 15,707 yalipokelewa na waombaji 1,005 waliitwa katika usaili kati yao, 200 walishinda na kuitwa kazini lakini baada ya kutoa tangazo la kuitwa kazini, malalamiko yalitolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa walioitwa katika ajira hizi ni watoto wa jamaa na ndugu.

 • UDA waandika historia Dar

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  UONGOZI wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na wamiliki wa daladala mkoani humo, wamesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano ili kushinda zabuni ya kuendesha Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART).

  Utiaji saini huo ulifanyika Dar es Salaam juzi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ukishuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia pamoja na na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Said Meck Sadiki.

  Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Ghasia alisema uamuzi uliochukuliwa na UDA pamoja na wamiliki wa daladala ni mfano wa kuigwa nchini.

  Alisema kuungana kwao pamoja, kutawajengea mazingira bora ya kuaminika zaidi na kutoa ushindani madhubuti dhidi ya kampuni za nje ambazo zitajitokeza kuomba kuendesha mradi wa DART.

  Alimpongeza Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Saimon Group, Bw. Robert Kisena na viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala mkoani humo kwa uamuzi huo wenye tija kwa Taifa kwani utaongeza ajira na kupunguza umaskini.

  Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mkutano uliokuwa na mafanikio makubwa uliofanyika jijini humo hivi karibuni katika Ukumbi wa Karimjee ulioandaliwa na Kamati Teule ya Wamiliki wa Daladala.

  Kwa upande wake, Bw. Sadiki alisema kuunganisha nguvu kwa wadau hao kutatoa fursa kwa Serikali kuwaunga mkono katika jitihada zake za kuboresha hali ya usafiri katika jiji hilo.

  "Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wazawa kwani haiwezi kutumia mabilioni ya fedha kujenga barabara hizo halafu mtu wa kuziendesha atoke nje, hii itakuwa aibu na dharau.

  "Kuungana kwenu, kutaishawishi Serikali baada ya kutangazwa zabuni, ianze kuwafikiria nyinyi kwa kuwapa kipaumbele kwani hii ni ishara kwamba, mmedhamiria kupambana katika zabuni," alisema Bw.Sadiki.

  Naye Bw. Kisena, alisema watafungua milango kwa wamiliki hao kununua hisa ambazo zitamwezesha mtu yeyote kuwa Mkurugenzi.

  "Tunatoa wito kwa wananchi mbalimbali, wajitokeze kununua hisa kwa wingi zaidi ili kuhakikisha tunaboresha huduma ya usafiri katika jiji hili," alisema Bw. Kisena.

  Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala mkoani humo (DARCOBOA), Sabri Mabrouk, alisema UDA ni kampuni yenye uwezo hivyo kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kuhakikisha zabuni inapotangazwa hakuna kampuni kutoka nje itakayoshinda.

  "Hakuna sababu ya kumwachia mtu kutoka nje aje kuendesha mradi huu, tukikusanya mitaji tukaungana na UDA, tutaweza kuendesha mradi huu kwani hauhitaji fedha nyingi sana, tukiamua tunaweza," alisema.

 • Meya wa CHADEMA asusia mbio za Mwenge

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  MEYA wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Japhary Michael kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesusia kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru katika manispaa anayoiongoza.

  Kutokana na kitendo hicho, kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Bi.Rachel Kasanda, alidai kusikitishwa na hali hiyo akisema Michael hakuwatendea haki wananchi anaowaongoza.

  "Mwenge huu si wa chama chochote cha siasa bali hii ni nembo ya Taifa, upo kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya wananchi," alisema.

  Alisema pamoja Michael kushindwa kutoa ushirikiano, mbio za Mwenge huo zimezindua barabara ambayo ipo Mtaa wa Shahili anaoishi Meya huyo ambako ana nyumba na duka labiashara.

  "Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi yake kutoshiriki katika mbio za Mwenge nchini tangu ulipowashwa Mei 2 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal Mjini Bukoba, mkoani Kagera," alisema.

  Bi. Kasanda alisema, Meya huyo hakupaswa kususia Mwenge wa Uhuru ambao unaleta maendeleo kwa Watanzania na barabara iliyozinduliwa katika mtaa huo inatumika na watu wote bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, rangi au dini.

  Hata hivyo, Michael ambaye baada ya uzinduzi wa barabara hiyo alikuwepo dukani kwake, alisema amewakilishwa na madiwani watatu wa chama chake.

  Alisema msafara wa Mwenge ulikuwa na madiwani wengine wa CHADEMA akiwamo Diwani wa Kata ya Kiusa, Stephen Ngasa hivyo hapakuwa na ulazima wa yeye kuwepo.

 • Mil. 90/- zatumika kutekeleza miradi Jiji la Mbeya

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  ZAIDI ya sh. milioni 90 zilizotengwa na Mfuko wa Jimbo mkoani Mbeya, zimetekeleza miradi 20 jijini humo kwa mwaka 2011/13.

  Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa ya shule za msingi, sekondari, vyoo, zahanati, viwanja na madawati.

  Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Maanga, mkoani humo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi kwa tiketi ya CHADEMA, alisema baadhi ya miradi iko katika hatua za awali na mingine imekamilika.

  Alisema shule zilizonufaika na fedha hizo kwa awamu ya kwanza ni Itagano iliyopo Kata ya Uyole na Ruanda ambapo sh. milioni 20, zilisaidia kufanikisha ujenzi wa majengo ya utawala.

  Miradi mingine ni ukamilishaji ujenzi wa madarasa shule za msingi Simike, Iduda, Nonde, Ikuti, Kalobe na sekondari Legico zilizopo katika Kata za Mabatini, Iduda, Nonde, Mbalizi Road, Majengo na Iyunga ambapo sh. milioni 30 zilitumika.

  Bw. Mbilinyi aliitaja miradi mingine iliyotelekezwa ni mradi wa ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa katika Kata ya Kalobe, ukarabati wa viwanja shule za msingi Mbata, Nzovwe na Ilolo kwenye Kata za Ghana, Nzovwe na Isanga ambapo fedha zilizotumika ni sh. milioni 7.5.

  Madawati 200 yalipelekwa katika shule za Juhudi, Ikuti, Itiji, Nero na Mwenge ambapo utekelezaji miradi ambayo inatokana na fedha za mfuko huo utakamilika Desemba mwaka huu.

  "Zipo changamoto nyingi za kisiasa katika kutekeleza miradi hii, hali hiyo ilichangia baadhi ya mambo kukwama kutokana na tofauti za kiitikadi na wasimamiziwa mfuko," alisema.

  Hata hivyo, Bw. Mbilinyi alisema kupitia nguvu ya wananchi, baadhi ya miradi kama ujenzi wa Daraja la Iyela ambalo linatumiwa kwa asilimia kubwa na wakazi wa Mbeya kwenda makaburini, limejengwa kutokana na shinikizo lake.

  Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Mjini, Bw. John Mwambigija, alisema wamejipanga kupata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2015.

  "Tumejipanga vyema katika chaguzi zijazo, CCM wasidhani kuwa tutawaachia jimbo hili badala yake tutaongeza madiwani na kuchukua Halmashauri ya Jiji la Mbeya liwe mikononi mwetu," alisema.

 • Foreplan yajitosa kutoa elimu ya fistula

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  SERIKALI imeahidi kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Foreplan ili kuhakikisha inamaliza tatizo la ugonjwa wa fistula kwa kutoa elimu ya ugonjwa huo katika mikoa mbalimbali.

  Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bw. Meshack Ndaskoi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mdahalo uliofanyika Dar es Salaam ili kujadili ukubwa wa tatizo hilo hasa maeneo ya vijijini.

  Alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na kuunga mkono juhudi zao za kumaliza tatizo la ugonjwa huo nchini.

  "Serikali peke yake, haiwezi kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya ndio maana imekuwa bega kwa bega na wadau zikiwemo taasisi kwa kuziunga mkono katika kampeni mbalimbali za kutokomeza magonjwa yanayoweza kuzuilika," alisema.

  "Zipo taasisi mbalimbali ambazo zimeanza kampeni za kutokomezaugonjwa huu na nyingine zinazoanza kama Foreplan, zitasaidia kuhakikisha ugonjwa huu nchini kwetu unabaki kuwa historia," alisema.

  Naye Mkurugenzi wa Mipango, Jinsia na Ushirikiano wa Foreplan, Bi. Zainab Aziz, alisema mdahalo huo ni mwendelezo wa midahalo mingine ya kuelimisha jamii kuhusiana na ugonjwa huo.

  Alisema kuna baadhi ya watu wenye fikra potofu kwa kuuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina kitu ambacho kinachangia kuongeza tatizo hilo.

  "Kutokana na fikra potofu za baadhi ya watu, Taasisi yetu imeamua kuandaa mdahalo ambao utawahusisha wadau mbalimbali wa afya ili waweze kujadili kwa pamoja sababu zinazosababisha ugonjwa huu na kutoa elimu kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini," alisema.

  Aliongeza kuwa, baada ya mdahalo huo taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu ya ugonjwa huo kupitia tamthiliya na burudani ili kumwezesha kila Mtanzania kupata elimu sahihi ya kujikinga na fistula.

  Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo, Dkt.Mwaka Juma, alisema taasisi hiyo pia itatoa elimu kwa wakunga wa jadi ili waweze kuelewa chanzo kinachosababisha ugonjwa huo.

  "Kwa kuwa taasisi yetu inajihusisha zaidi na masuala ya afya ya mama na mtoto, baada ya mdahalo huu itaendelea na kampeni ya kuielimisha jamii kuhusiana na athari zinazoweza kujitokeza kwa watu wenye tabia ya kutoa mimba," alisema Dkt. Mwaka.

  Dkt. Mwaka alisema, kampeni ya kuelimisha jamii juu ya madhara ya utoaji mimba, itawawezesha wasichana kuchukua hatua za kuachana na tabia hiyo na kutambua njia sahihi za kuzuia mimba zisizotarajiwa.

  Mdahalo huo uliandaliwa na taasisi hiyo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwepo wageni kutoka Mashirika ya Kimataifa UNDP, Wizara ya Afya na wadau kutoka taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya afya ya jamii.

kimataifa

Vikosi vya Iraq vyawakabili wapiganaji

Monday, August 25 2014, 0 : 0

 

WANAJESHI wa serikali ya Iraq wamesema wamelikabili shambulizi la wanamgambo katika kiwanda kikuu cha mafuta katika mji wa Beiji; na kuua wanamgambo kadhaa.

Kiwanda hicho kilichopo kaskazini mwa Iraq kimekuwa eneo la tukio la mapigano kadhaa kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita.

Hapo juzi mlolongo wa milipuko mitatu ya mabomu katika mji wa Kirkuk kaskazini mwa Iraq iliua takriban watu 18.

Vyombo vya habari vya Kikurdi vimesema maafisa wa kikosi cha kulinda amani cha Kikurdi, Peshemerga ni miongoni mwa waliouawa.

Kwa mujibu wa BBC, kundi la wapiganaji wa Kisunni-Islamic State-linashukiwa kutekeleza mashambulizi hayo.

Wapiganaji hao wa kikurdi Juni waliuteka mji huo wenye utajiri wa mafuta baada ya jeshi la Iraq kutoroka likihofia mashambulizi ya wapiganaji hao wa Kisunni.

Wakati huo huo, bomu lingine limelipuka katika mji wa Erbil, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la wakurdi.

Tukio hilo katika mji wa Erbil ni la kushangaza kwa kuwa ndio eneo lenye utulivu nchini Iraq.

Awali, mtu aliyejitoa muhanga aliua takriban watu wanane mjini Baghdad karibu na makao makuu ya ujasusi.

Jeshi la Afrika Mashariki kuanza kazi Desemba

Friday, August 22 2014, 0 : 0

NCHI 10 za ukanda wa Mashariki mwa bara la Afrika zimekubaliana kuunda kikosi cha pamoja cha askari jeshi na polisi.

Kikosi hicho kitakuwa tayari kuingilia kati mahali popote miongoni mwa nchi hizo ifikapo Desemba.

Azimio hilo lilitangazwa na wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo kwenye kikao chao kilichofanyika mjini Kigali, Rwanda.

Uamuzi huo ni jitihada za kukabiliana na matukio ya ukosefu wa usalama yanayosababishwa na makundi ya ugaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Uamuzi wa kuwepo kwa kikosi imara cha kukabiliana na migogoro uliazimiwa na Umoja wa Afrika ili kwamba ifikapo Desemba, mwaka ujao, kuwepo na vikosi vya aina hiyo kutoka kanda tano za bara la Afrika ikiwemo kanda ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo kutokana na usalama mdogo unaosababishwa na makundi ya kigaidi katika Kanda ya Mashariki mwa Afrika, viongozi wa nchi hizo 10 walikubaliana Juni mwaka huu kwamba ni lazima kiundwe kikosi cha pamoja cha jeshi kabla ya kumalizika Desemba, mwaka huu.

Sasa wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo wamepitisha kwa kauli moja kuanzishwa kwa kikosi hicho.

"Tulianza 2004 na leo ni 2014, kwa hiyo kwa miaka 10 tulikuwa tunatoa mafunzo kwa wale watakaojiunga na kikosi hicho, na tunaona tumefanya maandalizi ya kutosha kuweza kuanza Desemba," alisema Brigedia Jenerali Tai Gitwai kutoka sekretarieti ya mataifa hayo.

 • Wanane wanyongwa China kwa 'ugaidi'

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  CHINA imewanyonga watu wanane katika jimbo la magharibi la Xinjiang linalokaliwa na Waislamu wengi.

  Watu hao wamenyongwa baada ya kutiwa hatiani na mahakama ya mji wa Urumqi kwa makosa ya kufanya ugaidi.

  Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya China, watatu kati yao walikutwa na hatia ya kupanga mashambulizi katika Uwanja wa Tiananmen mjini Beijing Oktoba mwaka uliopita, ambapo watu watano waliuawa.

  Watu wengine watano walionyongwa walituhumiwa, miongoni mwa mambo mengine, kutengeneza mabomu na kuwashambulia maafisa wa serikali.

  Kwa mujibu wa DW, Jimbo la Xinjiang limekumbwa na wasiwasi kutokana na mgogoro wa muda mrefu kati ya Waislamu wa jamii ya Uighur na Wachina wa jamii ya Han.

  Serikali mjini Beijing imeimarisha kampeni dhidi ya wale inaowaita magaidi, tangu Mei, wakati washambuliaji waliporusha mabomu kwenye soko mjini Urumqi na kuua watu 43.

  Tangu wakati huo, mamia ya watu wameswekwa jela kwa vifungo virefu, huku baadhi wakipewa adhabu ya kifo.

 • Muingereza aambukizwa ebola

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  RAIA wa Uingereza anayeishi nchini Sierra Leone ameambukizwa virusi vya ugonjwa wa ebola, Idara ya Afya imethibitisha.

  Tangu Machi, zaidi ya watu 1,400 wameripotiwa kufa magharibi mwa Afrika.

  Idara ya Afya imesema raia wa kwanza Muingereza kuambukizwa ugonjwa huo alikuwa anaishi Sierra Leone.

  Kwa mujibu wa BBC, taifa hilo ni miongoni mwa mataifa ambayo yameathiriwa vibaya na ugonjwa huo.

  Iwapo atapewa matibabu nchini Uingereza mgonjwa huyo ana uwezekano mkubwa wa kupata nafuu kwa sababu hospitali za Sierra Leone zimejaa waathirika wa ugonjwa huo hatari ambao unaendelea kuenea kwa kasi.

  Eneo la kuwatenga wagonjwa tayari limebuniwa katika hospitali ya Royal Free mjini London.

  Mpaka sasa hakuna tiba ya ugonjwa huo, japokuwa dawa ya majaribio iliwasaidia raia wawili wa Marekani kupona huku maafisa watatu wa afya pia wakionesha dalili za kupata nafuu walipoitumia dawa hiyo nchini Liberia.

 • Bunge lashutumu wanamgambo

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  BUNGE jipya la Libya limeshutumu muungano wa wanamgambo ambao unajaribu kuuteka uwanja wa ndege wa mji wa Tripoli.

  Bunge hilo limeutaja muungano huo kuwa wa kigaidi na kuongezea kuwa vikosi vya taifa hilo vitakabiliana nao.

  Kwa mujibu wa BBC, muungano huo unashirikisha wanamgambo wa Kiislamu pamoja na wanamgambo kutoka mji wa Misrata.

  Msemaji wa wapiganaji hao amesema kuwa Bunge hilo ni haramu na kutaka kurudishwa kwa baraza la kitaifa lililotawaliwa na Waislamu.

 • Israel yaanza kuhujumiwa

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  MASHAMBULIZI mapya ya makombora kutoka Lebanon na Syria yamezua wasiwasi wa kusambaa vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.

  Usiku wa kuamkia jana, makombora matano yalifyatuliwa katika Milima ya Golan kutoka nchini Syria, lakini hayakuripotiwa kusababisha maafa au uharibifu.

  Kwa mujibu wa DW, Israel ililiteka eneo hilo la milima kutoka Syria wakati wa vita vya mwaka 1967.

  Juzi, wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali nchini Lebanon walifyatua makombora mawili kaskazini mwa Israel na kuharibu nyumba moja mjini Galilaya.

biashara na uchumi

Benki ya Exim yazidi kupiga jeki jamii

Monday, August 25 2014, 0 : 0

 

BENKI ya Exim Tanzania imekabidhi vyoo vya kisasa kwa Shule ya Msingi Kilakala iliyopo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ikiwa ni jitihada za benki hiyo kuboresha hali ya usafi na mazingira ya kujifunzia shuleni hapo.

Ujenzi huo wa matundu kumi ya vyoo na mfumo safi wa maji ni moja kati ya miradi ya kimaendeleo iliyotekelezwa na kugharamiwa na Benki ya Exim Tanzania katika shule hiyo ya Kilakala iliyo chini ya benki tangu mwaka 2012 ikiwa kama benki mlezi.      

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano shuleni hapo jana Mkuu wa Matawi/Cluster Head wa Benki ya Exim, Agnes Kaganda, alisema benki yake imeamua kupiga jeki mradi huo ikitambua umuhimu wa usafi kwa afya ya wanafunzi na walimu na mchango wake katika maendeleo kitaaluma kwa shule hiyo.

"Shule ilikuwa na maliwato yenye matundu nane tu ikiwa na wanafunzi 2,739. Kutokana na Benki ya Exim kuongeza matundu mengine 10, tunaamini kuwa hali hii sasa italeta ahueni kwa wote, walimu na wanafunzi hapa shuleni," alisema.

Alisema kuwa mbali na matundu hayo kumi, wavulana nao wana sehemu maalumu ya maliwato ikiwa na maji yanayotembea ili kuiweka maliwato katika hali ya usafi muda wote.

"Tunaamini kuwa, kwa kuboresha hali ya usafi ya shule kutasaidia kuzuia wanafunzi hasa wasichana kutoruka vipindi vya masomo ili kutafuta vyoo visafi au wanafunzi kutoambukizwa magonjwa mbalimbali. Hii itawasaidia wao kuelekeza zaidi jitihada zao katika masomo, na hivyo kuweza kufanya vizuri zaidi darasani," alisema Kaganda.

Alibainisha kuwa sasa ni juu ya uongozi wa shule na jamii inayoizunguka shule kuhakikisha kuwa maliwato hiyo inatumika vizuri ili iweze kutumika na wanafunzi wengine wanaoweza kujiunga na shule hiyo siku za usoni.

"Ningependa kuuasa uongozi wa shule na wanafunzi kuhakikisha kuwa maliwato hii inatunzwa na inabaki kuwa safi. Lengo hili litatimia tu endapo tutaweza kuiweka maliwato yetu katika hali ya usafi," aliongeza.

Alibainisha kuwa Benki ya Exim imekuwa ikiibadilisha shule taratibu tangu ilipokuwa benki mlezi, ambapo sasa shule hiyo inajivunia kuwa na maktaba ya kipekee, wanafunzi wakisoma wamekaa kwenye madawati yaliyotolewa na benki, na sasa shule ina mfumo nzuri wa maji safi, vikitajwa kwa uchache. Miradi yote ikifadhiliwa na benki kama sehemu ya shughuli mbalimbali za kijamii.

Naye, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Abdul Kuratasa, alipongeza jitihada za benki katika kufuatilia maendeleo ya shule tangu ilipoichukua kama benki mlezi na kusema kuwa sasa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kilakala wanafurahia matumizi ya vifaa vya kisasa kama shule nyingine za binafsi.

Alisema kuwa mchango huo wa maliwato ni moja kati ya hatua ambazo zinapaswa kuigwa na makampuni mengine ili kuboresha sekta ya elimu nchini.

"Naipongeza benki kwa jitihada zake kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya kujisomea ya shuleni hapa. Dhamira ya benki katika kusimamia maendeleo ya shule imekuwa thabiti tangu ilipoichukua shule yetu kuwa benki mlezi mnamo Agosti mwaka 2012.

"Tungependa kuishukuru benki kwa kutujengea maliwato na tunaahidi kuwa tutaitunza vyema kwa ajili ya wanafunzi wengine katika siku za usoni," alisema Kuratasa.

 

Waridhia korosho kuuzwa mfumo wa stakabadhi

Friday, August 22 2014, 0 : 0

 

WADAU wa zao la korosho wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma wameridhia kuuza korosho kupitia mfumo wa Stakabadhi ya mazao ghalani kuanzia msimu huu wa mwaka 2014/2015 zikiwa ni juhudi za kujiletea maendeleo tofauti na sasa ambapo wakulima hao wamekuwa wakipata hasara na kuwanufaisha wajanja wachache pindi wanapouza mazao yao kupitia mfumo wa soko holela.

Aidha wadau hao pia wamewapiga marufuku viongozi wa Vyama vya Msingi vya Wakulima wilayani humo kuendelea na utaratibu wa kwenda kukopa mikopo katika mabenki na kwenda kuwalipa fedha hizo kama malipo yao ya awali na kwamba hali hiyo pekee ndiyo itakayo saidia kuondoa manung'uniko kwa wakulima kulalamikia kuibiwa fedha zao.

Wajumbe hao waliendelea kubainisha kuwa fedha hizo za mikopo zimekuwa ni mzigo mkubwa kwa wakulima kutokana na kutakiwa kulipiwa riba kubwa ambazo hutozwa na mabenki hayo hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima kushindwa kulipwa malipo yao ya pili na ya tatu baada ya fedha hizo kuishia kulipia riba za mikopo hiyo katika mabenki ambayo hukopwa na viongozi hao wa vyama vya ushirika, mambo ambayo yamekuwa yakileta ugumu kwa wakulima kuupenda mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani.

Tamko hilo lilifikiwa katika mkutano uliohusisha wadau wa korosho wa kujadili mfumo wa kisheria wa kuuza mazao yao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.

Aidha katika kuhakikisha kuwa mfumo wa ununuzi wa mazao hayo kwa wakulima unafanikiwa, wakulima hao walikubali kutekeleza makubaliano ya kukusanya mazao yao katika maghala yaliyopo katika maeneo yao na kusubiri wanunuzi waende kununua hukohuko na kugawiwa fedha zao kulingana na idadi ya kilo alizozikabidhi.

Awali akitoa mada ya dhana ya bei dira na utekelezaji wake Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Bw.Mfaume Juma alisema kuwa mfumo huo ulianza kuhamasishwa msimu wa mavuno na mauzo ya korosho mwaka 2013/2014 na kuanza kutumika katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.

Alisema kuwa baadaye wilayani Tunduru mkoani Ruvuma msimu wa mwaka 2007/2008 na kwamba kabla ya hapo wanunuzi walikuwa wakinunua kupitia mfumo wa soko holela lakini wakiwa wananunua kupitia bei dira ambayo ilikuwa ikipangwa na Bodi ya Korosho Tanzania.

Bw.Juma aliendelea kufafanua kuwa pamoja na bodi hiyo kujipanga kusimamia utaratibu huo kwa uwazi kwa kuwashirikisha wawakilishi wa wakulima wakati wa kuuza korosho zao pia wameandaa mkakati maalumu na mazingira ya kusimamia uuzwaji wa korosho za Tunduru ikiwezekana hata kuhakikisha korosho hizo zinauzwa kwa utaratibu wa malipwani.

Alisema kuwa kwa tani 1 huuzwa hadi kwa dola za Marekani 1400, sawa na sh.2,240,000 tani moja sawa na kila kilo moja itauzwa kwa bei ya sh. 2,240 zikiwa ni juhudi za kumuondoa mtu wa kati yani Madalali na viongozi wa vyama vya ushirika mabavyo vimekuwa vikijinufaisha kupitia mgongo wa wakulima, Bw. Juma Aliendelea kueleza kuwa Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani kazi za vyama vya msingi ni kukusanya mazao na kuyatunza katika maghala ya chama,kupanga madaraja,kufungasha katika magunia yenye uzito sahihi, kusafirisha korosho hadi sokoni, kusimamia mauzo wakati wa minada na kuwagawia wakulima fedha zao.

Alisema kwamba mtindo wa kukopa fedha katika mabenki haupo katika utekelezaji wa mfumo huo na kwamba viongozi wabadhirifu katika vyama vyao wawatoe wakati wa uchaguzi na kuwaweka madarakani viongozi waadilifu.

Akifafanua matumizi ya mfumo huo Mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania, Bw.Athuman Nkinde alisema kuwa pamoja na mkakati huo wa kuwadhibiti walanguzi hao mfuko huo umetenga sh. bilioni 6 kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mtwara na Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema katika mpango huo kila kiwanda kimetengewa sh. bilioni 2 zikiwa ni juhudi za serikali kukuza soko la ndani ili kuwainua wakulima na kuwawezesha kuuza mazao yaliyosindikwa na kwamba, mkutano huo umelenga kuwajengea uwezo na kufungua upeo kwa wakulima na kuwawezesha wakulima kupata faida na kuiwezesha halmashauri kupata ushuru mkubwa na kuifanya halmashauri yao kujitosheleza katika bajeti zake za matumizi ya ndani.

 • Watanzania wapewa mbinu za kupanua soko

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  WATANZANIA wametakiwa kubadilika kwa kupenda kutumia bidhaa zinazokidhi viwango ili kupanua uwezo wa soko la bidhaa nchini.

  Akizungumza katika uzinduzi wa ufumbuzi wa vifaa vya umeme vinavyotoa hewa Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Panasonic Tanzania, Khalid Salim, alisema kuwepo kwa bidhaa zenye viwango kutawezesha nchi kuingia katika soko la Afrika Mashariki.

  Alisema ubora wa bidhaa katika soko utawezesha jamii kuweza kupata bidhaa imara zinazokidhi viwango kwa matumizi ya majumbani na maofisini.

  "Kutokana na mahitaji ya wananchi wengi Kampuni imebuni bidhaa hizo na kuanza kutoa huduma za kisasa kwa kuuza vifaa vya umeme vyenye ubora unaokubalika ili kuwezesha watumiaji kufurahia ubunifu huu," alisema.

  Alisema Panasonic imejipanga kuendelea kubuni bidhaa zenye ubora na usalama kwa watumiaji ili kupanua soko la ndani na nje ya nchi.

  Alivitaja vifaa ambavyo kwa sasa viko sokoni kuwa ni pamoja na feni, soketi breka, kebo na wiring.

  "Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na African Economic Outlook (AEO) uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa karibu asilimia 7 mwaka 2014", alisema.

  Naye Mkurugenzi wa Eco Solution Division Panasonic, Tatsuya Kumazawa, aliongeza kwamba bado kuna haja ya kuendelea kulisoma zaidi soko ili kufahamu hitaji zaidi.

  "Pamoja na Kampuni yetu kuingiza bidhaa hizi nchini kuna haja ya kuendelea kulisoma zaidi soko ili tuweze kuwafikia wananchi wote kwa kutoa huduma bora", alisema.

  Alisema tangu kuanza kwa kampuni hiyo imejijengea jina kwa kuwa na bidhaa bora na hivyo itahakikisha inaendelea kuimarisha huduma zake ili wananchi waweze kuzifurahia.

  Aliiomba serikali kuwaunga mkono na kuahidi kushirikiana kwa pamoja ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua.

 • Serikali haina fedha za kulipa fidia-Muhongo

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali haina fedha za kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo Mradi wa Umeme Vijijini (REA) unatekelezwa mkoani Kagera.

  Profesa Muhongo, alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa usambazaji umeme katika kijiji cha Katoke, wilayani Biharamulo, Kagera.

  Alisema Serikali haina fedha za kuwalipa wananchi fidia katika maeneo ya mradi wa REA ingawa ni haki yao, kwa sababu hiyo italazimika kuhamisha mradi na kuupeleka ambako wananchi hawahitaji fidia bali nishati ya umeme.

  Alisema kuwa, fidia ni utapeli na hakuna mahali ambapo fidia imetolewa (imelipwa ) kwa wananchi kesi zikaisha, hivyo wananchi waelezwe ukweli kuwa hakuna fedha za fidia. "Fidia ni haki yao, lakini hatuna fedha za kuwalipa.Sasa wafanye uamuzi, wanahitaji umeme au fidia.

  "Kama ni fidia wasubiri baada ya miaka 20.Na kwa sababu hiyo tutahamisha mradi tuupeleke maeneo wasikohitaji kulipwa fidia," alisema Profesa Muhongo.

  Alisema dhamira ya serikali ni kufuta umaskini na kuleta ajira mpya kwa kuwaunganishia wananchi umeme ambao utasaidia kukuza na kuboresha biashara zao, kilimo cha kisasa, kuboresha huduma za afya na elimu.

  Aidha alisema tatizo ni wananchi kukataa kulipa fedha za kuunganishiwa umeme ambazo ni sh 27,000 tu,na kufafanua kuwa taasisi za umma (ofisi za watendaji, shule na zahanati) na taasisi za kidini (makanisa na misikiti) zitaunganishiwa bure nishati hiyo.

  Profesa Muhongo, aliwataka Wahandisi nchini kuanzisha kampuni zao wafanye kazi za miradi mbalimbali ya ujenzi wa nishati ya umeme, badala ya kulalamika kuwa kazi nyingi wanapewa wageni badala ya wazawa.

  Aidha Mratibu wa mradi huo mkoani Kagera, Mhandisi Julius Kateti wa kampuni ya Urban and Rural Engineering Service Ltd, alisema mradi huo utagharimu sh. 98 bilioni na utakamilika Januari mwakani.

  Alisema zinahitajika nguzo 55,000 ili kukamilisha mradi huo na kampuni hiyo imeagiza nguzo nyingine kutoka nchini Uganda na Afrika Kusini.

 • Maonesho ya bidhaa za Kichina yamalizika

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  MAONESHO ya biashara za bidhaa za Kichina yamemalizika jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.

  Maonesho hayo ambayo yalikuwa yanahusisha bidhaa mbalimbali za Kichina, yamemalizika jana ambapo yalianza tangu Agosti 21 mwaka huu. Akizungumza Dar es Salaam jana, mmoja wa wafanyabiashara aliyeshiriki maonesho hayo, Paul John, alisema maonesho hayo kwa mwaka huu yameongezeka zaidi tofauti na miaka iliyopita.

  Alisema kuwa hata bidhaa zilizoletwa mwaka huu zimeongezeka zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali. John alisema kuwa pia katika maonesho hayo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwa na upungufu wa wateja katika siku ya kwanza, lakini baadaye waliongezeka.

  Alisema kuwa bidhaa zilizoletwa mwaka huu zimekuwa tofauti kwani kuna baadhi ni mpya kabisa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara.

  Alisema kuwa ana imani kubwa kuwa maonesho hayo yataboreshwa zaidi msimu ujao ikiwa ni pamoja na kuleta bidhaa mpya na zenye ubora zaidi.

  "Maonesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi pamoja na kuwa kuna changamoto mbalimbali tulizozipata, na hivyo tunatarajia kuwa bidhaa zitakazoletwa katika maonesho ya mwakani zitakuwa bora zaidi," alisema.

 • Maonesho ya bidhaa za Kichina yazinduliwa Dar

  Friday, August 22 2014, 0 : 0

   

  MAONESHO ya bidhaa za Kichina, yamezinduliwa jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.

  Maonesho hayo ambayo yanafanyika mwaka huu kwa mara ya tatu, yanatarajiwa kumalizika Agosti 24, mwaka huu.

  Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda, alisema kuwa maonesho hayo yanalenga kuendeleza na kukuza uchumi nchini.

  Alisema kuwa Wafanyabiashara mbalimbali watapata nafasi ya kukutana na wafanyabiashara kutoka nchini China kwa ajili ya kubadilishana mawazo ya kibiashara.

  Alisema kuwa kupitia ushirikiano uliopo kati ya China na Tanzania utaleta maendeleo zaidi ya kibiashara ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda mbalimbali ili kuweza kuongeza ajira kwa Watanzania.

  Waziri huyo alisema kuwa Serikali imepanga kudhibiti masuala ya uingizwaji wa bidhaa mbalimbali zisizokuwa na ubora, ili kuhakikisha uchumi unaimarika kwa kiasi kikubwa.

  Maonesho hayo kwa mwaka huu yanahusisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashine, magari, vifaa vya nyumbani, vifaa vya umeme pamoja na vifaa vya ujenzi.

  "Tunatarajia kuwa maonesho ya mwaka huu yataendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya China na Tanzania na hivyo pia Serikali inajipanga kwa ajili ya kuhakikisha hakuna bidhaa ambazo hazina ubora zinazoingia nchini," alisema.

michezo na burudani

Real Madrid 'wawapa somo' Watanzania

Monday, August 25 2014, 0 : 0

 

WACHEZAJI wa soka nchini wametakiwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, ili waweze kufanya vizuri katika mchezo huo ambao unapendwa na watu wengi duniani.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam juzi na nahodha wa timu ya magwiji wa Real Madrid, Andres Sabido mara baada ya kumaliza mchezo wao na timu ya Tanzania Eleven XI uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na magwiji hao wa Madrid kung'ara kwa mabao 3-1.

Alisema ili mtu awe mchezaji bora ni lazima awe na nidhamu ndani ya soka na nje ya mchezo huo, kwani mara nyingi wachezaji wengi wanasahau suala hilo.

Nahodha huyo alisema hali ya kujisahau husababisha mchezaji mzuri kushindwa kuendeleza kipaji chake na matokeo yake, baada ya muda mfupi kutoweka kwenye mchezo huo.

Akizungumzia mchezo huo uliokuwa na burudani ya aina yake, Sobido alisema amefurahishwa na hali ya mchezo kwa ujumla pamoja na mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo.

"Watanzania ni mashabiki wazuri wa mpira wa miguu tofauti na nilivyokuwa nafikiria, sijaamini kuwaona kwa wingi uwanjani hali iliyotoa faraja kwetu," alisema.

Kwa upande wake, Ruben dela Red ambaye ndiye aliyeifungia timu yake mabao yote matatu alisema aliweza kuusoma mchezo huo kwa haraka hususan kwa upande wa mabeki.

Alisema timu hiyo ya magwijiya Tanzania ni miongoni mwa timu nzuri ambazo amewahi kukutana nazo na kwamba kufunga kwake pia imekuwa ni bahati kwa kuwa wapinzani wao walikuwa wazuri na walipata nafasi nyingi.

Kwa upande wake mchezaji wa Tanzania Eleven XI, Boniface Pawasa alisema sababu za wao kufungwa ni kutokana na kutokuwa na mazoezi kama wenzao ambao walionekana kujiandaa vizuri.

Alisema walikuwa na muda mfupi wa kufanya mazoezi kwa pamoja kama timu hali iliyofanya washindwe kuelewa ndani ya muda mfupi.

Pawasa aliyewahi kuwika na Simba, alisema kuwa muda wao wa mazoezi pia ulikuwa ni mdogo na ndiyo maana walionekana kuchoka mapema kwenye mchezo huo, ingawa waliweza kufanikiwa kushambulia kila walipopata nafasi.

Hata hivyo beki huyo alisema kipigo hicho kwao ni sawa na ushindi, kwani wenzao wana uzoefu mkubwa wa kucheza mechi za kimataifa tofauti na wao.

Phiri:Sipo Simba kwa ajili ya kuifunga Yanga tu

Friday, August 22 2014, 0 : 0

 

BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutoa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara huku ikionesha miamba ya soka nchini Simba na Yanga kukutana Oktoba 12, mwaka huu Kocha Mkuu wa Simba Patrick Phiri amesema kwamba malengo yake kuja Simba si kuifunga Yanga tu bali ni kutaka kutetea ubingwa wa Bara ili timu hiyo ishiriki michuano ya kimataifa.

Akizungumza mjini hapa jana, Phiri alisema yupo Simba si kwa ajili ya Yanga tu, bali ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mechi zake zote za ligi kuu.

"Nipo Simba kwa ajili ya kuhakikisha timu yangu kila mechi inafanya vizuri ili tutetee ubingwa, Yanga ni sehemu ya mechi ambazo nataka kushinda, hivyo nataka kuhakikisha kila mchezo nashinda na kila mechi nitaipa umuhimu," alisema Phiri.

Alisema ingawa macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yapo pindi timu hizo zinapokutana pia atahakikisha na mchezo huo anafanya vizuri lakini malengo yake si kuifunga Yanga peke yake.

Akizungumzia kambi waliyoweka Zanzibar, kocha huyo alisema amefurahi kwani ni sehemu ambayo ina utulivu mkubwa na pia anapata nafasi nzuri ya kukinoa kikosi chake kwa umakini zaidi.

"Kwa sasa natafuta mechi za kirafiki kwa ajili ya kukipima kikosi changu ili tukirudi Dar es Salaam tuwe tumeiva zaidi," alisema kocha huyo raia wa Zambia.

Katika ratiba hiyo ya ligi kuu mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC wataanza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.

Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

 • Tanzania yaiadhibu Burundi 25-20

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  TANZANIA imefanikiwa kushinda mchezo wake wa pili wa mpira wa mikono dhidi ya Burundi mabao 25-20 katika michezo ya Majeshi na Utamaduni kwa Nchi za Afrika Mashariki uliochezwa Migombani mjini hapa.

  Katika mchezo huo Tanzania ambayo ilikuwa na uchungu wa kufungwa na Kenya katika mchezo wake wa kwanza, ilicheza kufa au kupona ili kuona makosa ya mwanzo hayajirudii tena.

  Mchezaji Hemed Saleh wa Tanzania alikuwa ndiye nyota wa mchezo kwa kupata pointi sita ambapo kwa upande wa Burundi, Nkongurutse Bra alipata pointi nne wakifungana na Mutungu Christian.

  Tanzania ambayo ni wenyeji wa michuano hiyo imeonekana kung'ara zaidi katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa kikapu na netiboli kwa wanawake.

  Mbali na mchezo huo, pia katika uwanja wa Gymkhana Uganda iliwafunga bingwa mtetezi wa mpira wa kikapu timu ya Jeshi kutoka Kenya kwa jumla ya vikapu 52-47.

  Katika mchezo huo, Ivan Rumanyika aliibuka kidedea kwa kujipatia pointi 25 akifuatiwa na Joseph Chuma aliyepata pointi 15 wote kutoka Uganda, wakati kwa upande wa Kenya alikuwa ni Bernard Mfutu aliyepata pointi 10 akifungana na Joseph Uwino.

  Kwa upande wa netiboli, Kenya iliifunga Burundi mabao 91-14, katika mchezo uliochezwa uwanja wa JKU Mjini Unguja.

  Katika mchezo huo Kenya iliwatumia wafungaji wake, Carolina Makocha aliyefunga magoli 60 na Mekasa Christian aliyefunga magoli 31, huku Burundi wafungaji wake walikuwa ni Nininahanzwe Gloriate, aliyefunga magoli 11 na Liyunkuru Diana alifunga magoli matatu.

  Kwa mpira wa miguu timu ya Kenya iliiadhibu vikali Burundi baada ya kuifunga mabaoi 4-2 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Amaan.

  Kenye ilijipatia mabao yake kupitia kwa Waruru Stephen dakika ya 54 na 87, Amwayi Kevin dakika ya tano na Brigon Brian dakika 57, wakati Burundi ilijipatia mabao yake kupitia kwa Mustafa Francis dakika ya 25 na Hakizimana Pascal dakika ya 14.

 • Miereka Tanzania waandaa mashindano Nyerere Day

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  CHAMA cha Miereka Tanzania 'AWATA' waandaa mashindano Nyerere Day yatakayofanyika Oktoba 14 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam.

  Akizungumza na Times fm Msemaji wa Awata Eliakim Melkzedeck anasema wameamua kuyafanya mashindano hayo kwa ajili ya kumuenzi baba wa Baba wa Taifa, Mwl.Julius K.Nyerere anayetimiza miaka 15 ya kifo chake.

  Melkzedeck alisema kwa sasa wapo kwenye uthibitisho wa kuvithibisha vilabu shiriki katika michuano ya mchezo huo ambapo kasi yake inaonekana kusuasua kutokana na kuweka kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kuthibitisha ushiriki wake.

   

  "Tumeweka kiasi cha shilingi laki mbili kama pesa ya kujiunga na chama ili kuweza kushiriki mashindano haya si pesa kubwa lakini naziomba klabu husika kujitahidi kutoa kwa wakati," alisema Melkzedeck.

  Alizitaja jumla ya vilabu vinane vinavyotarajia kushiriki kuwa ni pamoja na JKT, Ngome, Nervi, Magereza, Dar Combine, WWC, Na Mawa kutoka Morogoro huku vilabu viwili tu ndivo vilivyothibitisha ushiriki wake.

  Melkzedeck aliwata makocha wa kila kilabu kushirikiana vyema na timu yake ili kuyafanya mashindano hayo kuwa na mvuto na yaina yake ili kuweza kuleta ushindani kwa kila klabu machoni mwa mashabiki wake.

 • Waamuzi watakiwa kuacha upendeleo

  Monday, August 25 2014, 9 : 27

   

  WAAMUZI wanaochezesha netiboli katika michuano ya Majeshi ya Afrika Mashariki inayoendelea visiwani hapa, wametakiwa kuacha upendeleo kwa timu yoyote katika michezo hiyo.

  Kocha Mkuu wa timu ya Kenya, Millicent Busolo alilazimika kulalamika mara baada ya timu yake na Uganda mabao 30-28.

  Kocha huyo alisema katika michuano hiyo kuna baadhi ya waamuzi wamekuwa wakionesha upendeleo kwa baadhi ya timu wanazozipenda.

  Alisema ikiwa Afrika Mashariki moja ni lazima waamuzi hao wajaribu kubadilika, kwani hawakuja hapa kwa ajili ya kuchafuana bali ni kuendeleza uhusiano mwema kati ya nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

  "Hapa hatukuja kwa kuharibiana ni lazima haki itendeke, kwani sisi sote ni wa moja na tunahitaji kutendewa haki kunapokuwa na adhabu kutolewe adhabu na panapostahiki kuchezwa basi kuchezeshwe vizuri," alisema.

  Hata hivyo akizungumzia viwango vya waamuzi hao, kocha huyo alisema kuna wengine hawana viwango vya kuweza kuchezesha michuano hiyo.

  Michuano hiyo ya Majeshi na Utamaduni inashirikisha nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo yameanza kutimua vumbi Agosti 21 mwaka huu.

  Kenya tayari imeshacheza michezo miwili na kufungwa mmoja na kushinda mmoja dhidi ya Burundi, imebakiza michezo miwili ambao mmoja itacheza leo na Tanzania na mwingine itacheza kesho na Rwanda.

  "

 • Mchezaji apigwa uwanjani, afariki dunia

  Monday, August 25 2014, 0 : 0

   

  MCHEZAJI wa timu ya soka ya JS Kabylie ya Algeria, Albert Ebosse (24) amefariki dunia baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Algeria kati ya timu yake na wapinzani wao USM Alger.

  Ebosse ambaye ni raia wa Cameroon amefariki baada ya kupigwa na kitu kichwani mwake kilichorushwa kutoka kwa mashabiki mwishoni mwa mechi hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

  Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mshambuliaji huyo ndiye aliyeifungia timu yake bao pekee katika mechi hiyo ambayo, JS Kabylie ilifungwa mabao 2-1.

  Habari hizo zilieleza kuwa kitu kilichomgonga kichwani mchezaji huyo kilirushwa baada ya mechi kukamilika, wakati ambapo wachezaji walikuwa wanarudi katika vyumba vya kujiandaa.

  Kutokana na kifo hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Algeria ameagiza kuanzishwa uchunguzi kuhusu mauaji hayo.